UINGEREZA

Newcastle United yatangaza Mshambuliaji wake Demba Ba yupo njiani kujiunga na Chelsea

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Senegal Demba Ba anatarajiwa kujiunga na Chelsea akitokea Newcastle United
Mshambuliaji wa Kimataifa wa Senegal Demba Ba anatarajiwa kujiunga na Chelsea akitokea Newcastle United REUTERS/Darren

Klabu ya Chelsea ya Uingereza ipo katika hatua za mwisho za kumnasa Mshambuliaji wa Kimataifa wa Senegal anayekipiga kwenye timu ya Newcastle United Demba Ba aliyetengaza uamuzi wake wa kuondoka.

Matangazo ya kibiashara

Kocha Mkuu wa Newcastle Alan Pardew ndiye amethibitisha kuwepo wa mazungumzo baina ya Ba na klabu ya Chelsea ambao inasaka kwa udi na uvumba saini yake ili ajiunge nao mwezi huu wa Januari.

Ba ameruhusiwa kuongea na Chelsea kama ambavyo kifungu kimoja wapo kwenye mkataba wake kinavyoeleza na hivyo kuna kila dalili msahambuaji huyo akavaa jezi yenye rangi ya bluu mwazi huu.

Pardew baada ya mchezo wa kichapo kutoka kwa Everton akawaeleza wanahabari ana imani mpango wa Ba kuondoka utakamilika mapema na hana uhakika kama atarudi tena na kuwepo kwenye kikosi chake.

Kocha Pardew amesema wataendelea kusonga mbele licha ya kumpoteza Ba kwenye kikosi chake huku akiamini hakuna mchezaji ambaye anaweza akawa ana kipaumbele zaidi ya klabu hiyo kwa sasa.

Pardew ambaye alifanya kila linalowezekana kuhakikisha anambakiza Ba lakini anaonekana kushindwa kufanya hivyo kutokana na mshambuliaji huyo kutokuwa na raha baada ya kukosa namba ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza.

Ba amefunga magoli kumi na tatu katika Ligi Kuu nchini Uingereza msimu huu na alilazimika kuachwa kwenye kikosi cha Newcastle kilichocheza na Everton ili afanye mazungumzo na Chelsea.

Ba amefunga magoli thelathini na sita tangu ajiunge na Ligi Kuu nchini Uingereza mwaka 2011 huku akizidiwa na washambuliaji wawili ambao ni Robin Van Persie mwenye magoli sitini na nne na Wayne Rooney mwenye magoli arobaini na nne.