Afrika Kusini

Afrika Kusini yatangaza kuwa Tayari kuhodhi michuano ya kuwania Ubingwa Barani Afrika

Waziri wa Michezo nchini Afrika kusini,Fikile Mbalula
Waziri wa Michezo nchini Afrika kusini,Fikile Mbalula

Waziri wa Michezo nchini Afrika Kusini Fikile Mbalula ametangaza kuwa taifa hilo liko tayari kabisa kuandaa michuano ya kuwania ubingwa wa Afrika katika mchezo wa soka utakaoanza tarehe 19 mwezi huu.

Matangazo ya kibiashara

Mbalula amesema maandalizi yote yamekamilika na hata michuano hiyo ikianza wakati wowote kuanzia hivi sasa, mambo yote yatakwenda kama ilivyopangwa kwa sababu viwanja vyote viko katika hali nzuri.
 

Timu ya taifa ya Bafana Bafana itaanza kinya'nga'nyiro hicho dhidi ya Cape Verde kabla ya kumenyana na Morroco na Angola katika kundi la A.
 

Tayari idadi kubwa ya tiketi zimekwishauzwa kabla ya kuanza kwa michuano hiyo huku wito ukitolewa kwa mashabiki kujitokeza kwa wingi kushuhudia michuano hiyo.
 

Mashabiki wa soka nchini humo wanasema wanamatumaini makubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo ya kushinda taji hilo licha ya kufungwa na Nowray bao 1 kwa 0 katika mchauano wa kimataifa wa kirafiki.
 

Makocha wa timu mbalimbali zitakazoshiriki katika mashindano hayo wameshataja vikosi vyao vya mwisho tayari kwa michuano hiyo ikiwemo Zambia mabingwa watetezi ambao watafungua mchuano wao dhidi ya Ethiopia.
 

Wachambuzi wa soka nchini Nigeria wanasema, Super Eagles huenda ikamaliza katika timu tatu bora katika mashindano hayo kutokana na kikosi cha vijana chipukizi ambacho kocha Stephen Keshi amekitaja.
 

Miongoni mwa wachezaji watakaowakilisha Nigeria katika michuano hiyo ni pamoja na John Obi Mikel , Victor Moses wanaochezea klabu ya Chelsea nchini Uingereza na Ikechukwu Uche anayecheza katika klabu ya Villarreal huko Hispania.