Michezo-AFCON

Bingwa wa AFCON kujulikana leo nchini Afrika Kusini

Hatimaye fainali za kombe la Mataifa ya Afrika AFCON zinatarajia kufikia tamati jumapili hii kwa mechi ya fainali kati ya Burkina Faso na Nigeria katika dimba la Taifa mjini Soweto huko nchini Afrika kusini.

REUTERS/Mike Hutchings
Matangazo ya kibiashara

Nigeria au The Super Eagles wametinga katika hatua hii baada ya kuonyesha kiwango cha juu zaidi msimu huu ambapo pia ilifanikiwa kuwacharaza Mali mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali.

Burkina Faso wao wanatinga katika fainali baada ya kuwazamisha Ghana katika mechi ya nusu fainali kwa mabao 4-3 wakifanikiwa kupachika mikwaju mitatu ya penati baada ya dakika 120 za awali kumalizika kwa sare ya 1-1.

Burkina Faso kwa upande wao wamesema wanaamini wataibuka na ushindi dhidi ya Nigeria kutokana na kutoka nayo sare ya 1-1 katika hatua ya makundi.

Tambo zote hizo zitapata majibu baada ya mtanange wa fainali kumalizika hii leo ambapo macho na masikio ya mashabiki wa soka yameelekezwa huko nchini Afrika Kusini kujua nani atarithi taji hilo toka kwa mabingwa wa msimu uliopita Zambia ambapo waliishatolewa katika michuano hiyo.