Nigeria ndio mabingwa wa Afrika katika mchezo wa soka
Nigeria ndio mabingwa wa soka barani Afrika baada ya kuifunga Burkinafaso bao 1 kwa 0 katika fainali ya dimba la mataifa ya Afrika iliyofanyika jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini Jumapili usiku.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Sunday Mba ndiye aliyeifungia Super Eagles bao hilo la ushindi kabla ya kumalizika kwa kipindi cha kwanza cha mchuano huo waliouthibiti kwa kiasi kikubwa.
Ushindi wa Nigeria ni watatu katika historia ya mashindano haya ambayo wameshiriki mara 17 na kunyakua ushindi mwaka 1980, 1994 na sasa mwaka 2013 baada ya ukame wa miaka 19.
Mbali na wachezaji, maelfu ya mashabiki wa Super Eagles walikusanyika karibu na uwanja wa taifa mjini Lagos kuishangilia timu yao ambayo ilikuwa imekosa kombe hilo kwa kipindi kirefu.
Burkinafaso ambayo ilifika fainali kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano haya ilionekana kulinda lango lao kwa kipindi cha dakika 20 za mwanzo kabla ya kuanza kulisaka lango la Nigeria bila mafanikio kutokana na uthibiti wa hali ya juu ulioneshwa na wachezaji wa Super Eagles katika safu ya kati iliyoongozwa na John Obi Mikel na Elderson Echiejile.
Nigeria iliponea chupuchupu katika dakika ya 73 baada ya mkwaju wa mshambulizi Prejuce Nakoulma kuokolewa na na kipa Vincent Enyeama.
Jonathan Pitroipa mshambulizi matata wa Burkinafaso ambaye alitajwa kuwa mchezaji bora katika mashindano hayo na ambaye alikuwa anategemewa sana na kikosi chake alikabwa sana na walinzi wa Nigeria na kushindwa kuisaidia timu take kupata ushindi.
Kocha wa Nigeria Stephen Keshi ameweka historia kwa kuwa Mnaigeria wa kwanza ambaye pia aliwahi kuichezea timu yake na kunyakua kombe hilo mwaka 1994 alipokuwa nahodha na pia anakuwa Mwafrika wa pili baada ya Mahmoud El Gohary aliyeiongoza Misri mwaka 1959 kuwahi kuichezea timu yake na kuwa kocha na kuishindia nchi yake taji hili.
Nigeria sasa itawakilisha bara la Afrika katika mashindano ya Mashirikisho ya soka kutoka mabara mbalimbali duniani nchini Brazil mwezi wa Juni mwaka huu.