SOKA

Kocha wa Nigeria Stephen Keshi asema hatajiuzulu

Kocha wa timu ya taifa ya soka ya Nigeria Stephen Keshi amesema kuwa amebadilisha uamuzi wake wa kujiuzulu wadhifa wake baada ya kuiongoza Super Eagles kunyakua taji la michuano ya Mataifa bingwa barani Afrika.

Matangazo ya kibiashara

Keshi amesema ataendelea kuifunza timu hiyo baada ya serikali kuingilia kati suala hilo na tayari wamekwishaafikiana na shirikisho la soka nchini humo NFF.

Kocha huyo ameongeza kuwa wakati wa michuano hiyo alikuwa anapata kashfa nzito kutoka kwa viongoizi wa soka nchini humo na kueleza kuwa ushindi walioupata ulikuwa ni kwa neema za Mungu.

Keshi mwenye umri wa miaka 51 amesisitiza kuwa baada kuwasilisha malalamishi kwenye Wizara ya Michezo nchini humo amefikia uamuzi wa kuendelea na kazi ya kuwafunza mabingwa hao wa Afrika kazi aliyoianza mwaka 2011.

Siku ya Jumatatu Keshi alitangaza kupitia redio ya Afrika Kusini SABC kuwa alikuwa amejiuzulu kutokana na mtafaruko kati yake na viongozi wa shirikisho la NFF.

Rais wa Nigeria Goodluck Jonathan amekutana na wachezaji wa Nigeria jijini Abuja na kuwasifu katika juhudi zao za kuleta kombe hilo la Afrika nyumbani.

Jonathan ameongeza kuwa vijana wa Super Eagles wameiletea sifa Nigeria.
Nigeria walishinda taji hilo kwa mara ya tatu katika histiria ya michezo hiyo baada ya kuishinda Burkinafso bao 1 kwa 0 wakati wa fainali iliyochezwa nchini Afrika Kusini Jumapili iliyopita.