Soka

Shirikisho la soka nchini Uganda FUFA lakanusha kuwa kocha wa Cranes anaelekea Kenya

Shirikisho la soka nchini Uganda FUFA, limekanusha taarifa kuwa kocha wa timu ya taifa ya kandanda ya Uganda Cranes Bobby Williamson huenda akajiuzulu na kuhamia nchini Kenya kuinoa Harambee Stars.

Matangazo ya kibiashara

Gazeti moja la kila siku nchini Kenya siku ya Jumanne liliandika kuwa Williamson raia wa Scotland ambaye amekuwa akiifunza Cranes kuanzia mwaka 2008 alikuwa katika mazungumzo ya siri na viongozi wa shirikisho la soka nchini Kenya FKF kuhusu uwezekano wake wa kupewa kazi hiyo.

Shirikisho la soka nchini Uganda FUFA limesisitiza kuwa taarifa hizo si za kweli na wala kocha huyo hana mpango wa kuachana na Uganda Cranes kwa sasa.

Aidha, FUFA imeeleza kuwa Kocha Bobby kwa sasa anakiandaa kikosi cha Cranes kumenyana na  Liberia katika mchuano wa kufuzu kwa mashindano ya kombe la dunia mwaka ujao nchini Brazil.

Nchini Kenya, duru zinasema kuwa shirikisho la soka nchini humo linatarajiwa kumtangaza kocha mpya wiki ijayo.

Inaelezwa kuwa  Adel Amrouche  raia kutoka Ubelgiji huenda akarithi mikoba ya Mfaransa Henri Michel aliyejiuzulu mwezi mmoja baada ya kutofautiana na viongozi wa soka nchini humo mwaka uliopita.

Harambee Stars inajiandaa kumenyana na  Nigeria katika mchuano wa kufuzu kuwa kombe la dunia mwezi ujao.