FIFA

Cote d'Ivoire yasalia kuwa timu bora ya soka barani Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Cote dvoire licha ya kubanduliwa nje katika awamu ya robo fainali ya michuano ya kombe la mataifa bingwa barani Afrika iliyomalizika huko Afrika Kusini wiki iliyopita , inasalia kuwa timu bora barani Afrika na ni ya 12 duniani kwa mujibu wa orodha ya hivi punde iliyotolewa na shirikisho la soka duniani FIFA.

Matangazo ya kibiashara

Black Stars ya Ghana ambayo ni ya 19 duniani, ni ya pili barani Afrika katika msururu huo na pia ni  timu ambayo ilifika katika awamu ya nusu fainali ya michuano ya kombe la mataifa ya Afrika.

Super Eagles ya Nigeria ambayo ndio mabingwa wa Afrika katika mchezo wa soka wanaorodheshwa katika nafasi ya 30 duniani na ni  wanne barani Afrika nyuma ya Mali ambayo inashikilia nafasi ya tatu na ya 25 duniani.

Harambee Stars ya Kenya imepanda nafasi moja juu na sasa ni ya 126  duniani kutoka 127 baada ya ushindi wa mchuano wake wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya Libya walioshinda mabao 3 kwa 0.

Katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati, Uganda wanaongoza wakifuatwa na Ethiopia, Burundi ni tatu huku Kenya ikiwa ya nne ikifuatwa na Tanzania.

Duniani, Hispania bado inaongoza ikifuatwa na Ujerumani, Argetina ni ya tatu huku Uingereza ikipanda nafasi mbili juu na sasa inashikilia nafasi ya nne katika msururu huo wakati Italia iliyoshuka nafasi moja chini ikifunga tano bora.

Mataifa yaliyopanda katika orodhaa hii ya FIFA yanatokana  na ushindi waliopata wakati wa michuano ya kimataifa ya kirafiki ikiwemo Uingereza iliyoishinda Brazil mabao 2 kwa 1 wiki iliyopita.