FIFA

FIFA kuwachunguza wachezaji wanaotumia dawa za kusisimua misuli

Shirikisho la soka duniani FIFA limetangaza siku ya Ijumaa kuwa kila mchezaji atahitajika kuonesha rekodi ya vipimo kuthibitisha kuwa hajashiriki wala hatumii dawa za kusimumua misuli.

Matangazo ya kibiashara

FIFA imesema a vyeti hivyo vitaanza kutumiwa wakati wa michuano ya kuwania taji la Mashirikisho duniani itayoandaliwa nchini Brazil kama njia mojawapo ya kupambana na utumizi wa dawa za kusisimua misuli miongoni mwa wachezaji.

Viongozi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulika na uzuiaji wa kutumia dawa hizo baina ya wachezaji WADA walikutana katika makao makuu ya FIFA mjini Zurich nchini Uswisi na kufikia uamuzi huo na FIFA.

Afisaa Mkuu wa FIFA anayeshughulika na maswala ya afya katika Shirikisho hilo Michel D'Hooghe amesema kuwa FIFA ndilo shirikisho la kwanza kuanza kutekeleza mpango huo unaonuiwa kusafisha michezo duniani.

FIFA imeongeza kuwa itaanza kutekeleza mpango huo kwa kuwapima mkojo na damu wachezaji kubaini  ukweli wa mambo na kupigana na matumizi wa dawa hizo.

Jaribio la mpango huu kuwapima wachezaji lilianza mwaka 2002 wakati wa michuano ya kombe la dunia na kubainika kuwa wachezaji wote walikuwa katika hali nzuri.

Mbali na soka, mchezo wa riadha umekuwa ukikumbwa na tatizo hili la wanariadha kutumia dawa hizo kuvuliwa mataji.

Mwaka uliopita, aliyekuwa bingwa wa mashindano ya kuendesha baiskeli ya Tour De France Lance Amstrong raia wa Marekani alivuliwa mataji yake yote baada ya kubainika kuwa alikuwa anatumia dawa za kusisimua misuli wakati wa mashindano hayo.