UINGEREZA

Manchester City na Chelsea washinda kwa ushindi mnono michezo yao ya Kombe la FA

Wachezaji wa Chelsea wakishangilia mmoja ya magoli waliyofunga katika mchezo wao dhidi ya Brentford
Wachezaji wa Chelsea wakishangilia mmoja ya magoli waliyofunga katika mchezo wao dhidi ya Brentford

Klabu ya Manchester City imefanikiwa kutinga hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Chama Cha Soka nchini Uingereza FA baada ya kuibuka na uhsindi mnono wa magoli 4-0 mbele ya Leeds United. Manchester City ambao ni Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu nchini Uingereza walionekana kukamia mchezo huo uliopigwa katika Dimba la Etihad kwani dakika tano zilitosha kuwafanya kupata goli la kuongoza kupitia Yaya Toure.

Matangazo ya kibiashara

Mabingwa hao watetezi ambao wapo pointi 12 nyuma ya vinara wa Ligi Kuu nchini Uingereza Manchester United waliendelea kuonesha hasira zao baada ya kupata goli la pili kupitia Sergio Aguero kwa mkwaju wa penalti.

Leeds ambao waliwaondoa Tottenham kwenye uwanja wa Elland Road walionekana kuzidiwa zaidi baada ya Manchester City kupata magoli mengine mawili kupitia Carlos Tevez na Sergio Aguero.

Matokeo hayo yameondoa uvumi uliokuwa unatanda huenda Kocha Roberto Mancini angetimuliwa iwapo angeondoshwa kwenye hatua hiyo ya mtoano wa Kombe la Chama Cha Soka FA.

Mabingwa watetezi wa Kombe hilo Chelsea nao wakiwa nyumbani Stamford Bridge wakafanikiwa kusonga mbele baada ya kuishusha kipigo Brentford kwa jumla ya magoli 4-0 katika mchezo huo.

Chelsea walianza kupata goli la kwanza kipindi cha pili kupitia Juan Mata kabla ya mshambuliaji Oscar hajafunga goli la pili na kuanza kuipa matumaiani The Blues kuibuka na ushindi.

The Blues waliuendelea kuonesha kiu yao ya kutaka kuibuka na ushindi baada ya kufunga magoli mengine mawili kupitia Kiungo mkongwe Frank Lampard na Nahodha John Terry na kuhitimisha karamu yao.

Mashindano ya FA yanatarajiwa kuendelea hii leo ambapo Manchester United watakuwa na kibarua mbele ya Reading kusaka tiketi ya kutinga hatua ya Robo Fainali ya mshindano hayo makongwe zaidi.

Chama Cha Soka nchini Uingereza FA kimeshatoa ratiba ya hatua ya robo fainali ambapo kama Chelsea wakishinda mchezo wao dhidi ya Middlesbrough watakuwa na kibarua mbele ya mshindi kati ya Manchester United na Reading.

Michezo mingine inatarajiwa kushuhudia Millwall wakicheza na Blackburn Rovers huku Manchester City wakikabiliana na Barnsley wakati mpambano mwingine utawakutanisha Wigan Athletic dhidi ya mshindi kati ya Oldham Athletic na Everton.