UINGEREZA

Roberto Mancini ajigamba kuwa Kocha Bora zaidi nchini Uingereza katika kipindi cha miezi 15 iliyopita

Kocha Mkuu wa Manchester City Roberto Mancini amejigamba kuwa yeye ndiyo Kocha bora zaidi nchini Uingereza katika kipindi cha miezi kumi na mitano sasa na hawezi kutimuliwa. Kauli ya Mancini imekuja kipindi hiki ambacho amekuwa akikosolewa zaidi ya wadau wa soka akiwemo Mchezaji wa zamani wa Manchester City Danny Mills ambaye anaamini wakati wa kufanya mabadiliko ya kocha ni sasa.

Kocha Mkuu wa Manchester City Robert Mancini aliyetangaza kuwa bora zaidi ya makocha wengine kwa kipindi cha miezi 15
Kocha Mkuu wa Manchester City Robert Mancini aliyetangaza kuwa bora zaidi ya makocha wengine kwa kipindi cha miezi 15
Matangazo ya kibiashara

Mancini aliyejiunga na Manchester City mwaka 2009 kuchukua nafasi ya Mark Hughes amejigamba kwa kipindi cha miezi 15 amekuwa ni bora zaidi kutokana na mafanikio waliyonayo klabu yake.

Kocha huyo raia wa Italia mwenye kiburi amesema kwa kipindi chote ambacho yupo Manchester City ameweza kushinda Kombe la Ligi, Kombe la Chama Cha Soka FA pamoja na Ngao ya Jamii.

Mancini amesema hakuna Kocha ambaye ameweza kuchukua mataji kama ambayo yeye ameyatwa ndani ya Uingereza hivyo inadhihirisha wazi kabisa ubora wake dhidi na makocha wengine.

Kocha huyo amesema mengi yamekuwa yakisemwa juu yake na amekuwa akikosolewa kupita kiasi lakini ataendelea kuwa Kocha wa Manchester City kutokana na ubora alionao na hawezi kutimuliwa.

Wakosoaji wa Mancini akiwemo Danny Mills wanaamini kiasi ambacho amekitumia Kocha huyo cha pauni milioni 285 hakiendani na mafanikio aliyoyapata na hivyo inafaa aondoke na nafasi yake ichukuliwe na mtu mwingine.

Manchester City ambao wapo nje ya Mashindano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa na pointi kumi na mbili nyuma ya vinara wa Ligi Manchester United inakabiliwa na wakati mgumu wa kuweza kutetea ubingwa wao.

Katika hatua nyingine Kocha Mancini ameonesha kufurahishwa na kiwango cha Mshambuliaji wake Sergio Aguero ambacho amekionesha dhidi ya Leeds United na kufunga magoli mawili.

Mancini amekiri kama Aguero atakuwa anafunga magoli mengi kama hivyo basi ni wazi kabisa mbio za kusaka Ubingwa wa Ligi Kuu nchini Uingereza bado hazijaisha na wana matumaini ya kuchukua Ubingwa huo.