CHINA

Klabu ya Shanghai Shenhua yapigwa faini kwa kupanga matokeo huku wachezaji 33 wakifungiwa maisha

Chama Cha Soka nchini China SFC kimewafungia wachezaji 33 pamoja na maofisa kwa maisha yao yote kujishughulisha na masuala ya mpira wa miguu baada ya kukutwa na hatua ya kupanga matokeo. Uchunguzi wa SFC umedumu kwa kipindi cha miaka mitatu kuwabaini wale ambao wanashiriki kwenye vitendo vichafu vya upanagaji wa matokeo vilivyosababisha kuchafuka kwa sifa njema ya mpira wa miguu nchini China.

Kiongozi wa Klabu ya Shanghai Shenhua akiwa mbele ya Bodi kujitetea na tuhuma za upangaji wa matokeo
Kiongozi wa Klabu ya Shanghai Shenhua akiwa mbele ya Bodi kujitetea na tuhuma za upangaji wa matokeo
Matangazo ya kibiashara

Bodi ambayo ilikuwa inashughulikia uchunguzi imeshusha rungu zito kwa wachezaji hao pamoja na maofisa ambao wamekutwa na hatia ya moja kwa moja ya kushiriki kwenye upangaji wa matokeo.

Kipindi cha miaka ya hivi karibuni China imekuwa ikifanya kila linalowezekana kusafisha mchezo wa mpira wa miguu ambao umegubikwa na kashfa mbalimbali ikiwemo kubwa ya upangaji wa matokeo.

Klabu ya Shanghai Shenhua ni miongoni mwa waathirika wakubwa wa maamuzi haya kwani imelimwa faini ya pauni 103,000 baada ya kubainika nayo ilihusika kwenye mchezo mchafu wa upangaji wa matokeo.

Bodi hiyo imewapoka ubingwa Shanghai Shenhua ambao waliutwaa mwaka 2003 baada ya kubainika miongoni mwa michezo yao wakielekea kutwaa taji hilo ilipangia matokeo na hivyo hawana uhalali wa kuwa na ubingwa huo.

Adhabu hiyo imezigusa Klabu 12 ambazo kuna zile ambazo zimepingwa faini pekee lakini kuna nyingine zinazolazimika kukatwa pointi kwa makosa ya upangaji wa matokeo katika michezo yao.

Miaka iliyopita zaidi ya maofisa 50, waamuzi na wachezaji nchini China walishawahi kufungwa jela kutokana na makosa mbalimbali kwenye mchezo wa mpira wa miguu na sasa sheria inaanza kuchukua mkondo wake tena.