UINGEREZA

Kocha Arsene Wenger akanusha madai ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili kusalia Arsenal

Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger akanusha madai ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili
Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger akanusha madai ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili

Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger amekanusha ripoti zinazomhusisha yeye kupewa mkataba wa miaka miwili kuendelea kuinoa timu hiyo kipindi hiki ambacho amekuwa akikabiliwa na matokeo mabaya. Wenger kwenye mkutano wake na waandishi wa habari amekanusha vikali taarifa hizo na kuita uzushi unaosambazwa na watu wasiojua ukweli wa kile ambacho kinaendelea ndani ya Klabu ya Arsenal.

Matangazo ya kibiashara

Kocha huyo amesema anastahili kupewa heshima yake na sifa zake kutokana na kile ambacho amekifanya kwa muda wote anaokinoa kikosi cha Srsenal badala ya kuendeleza mashambulizi dhidi yake.

Wenger amesema wengi wanamkosoa kutokana na kuondolewa kwenye Kombe la Chama Cha Soka nchini Uingereza FA dhidi ya Blackburn Rovers ambapo wengi wamekuwa wakidai hatilii maanani mashindano hayo.

Kocha huyo alionekana kuchukizwa na maswali ya wanahabari ambayo yalikuwa yamelenga mchezo wao wa jumamosi dhidi ya Blackburn Rovers na yeye akawataka waangalie mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Bayern Munich.

Mfaransa huyo amesema wengi wanamtaka apange kikosi kimoja kwenye kila mchezo na anapofanya mabadiliko kisha matokeo kuwa mabaya basi lawama zimekuwa zikimwangukia yeye.

Wenger amewataka washabiki kuachana na malumbano yanayoendelea na badala yake kukaa pamoja ili kujenga uimara wa kikosi cha Arsenal hasa kipindi hiki ambacho wanataraji kucheza na Bayern Munich.

Kocha Wenger hajashinda kombe lolote tangu mwaka 2005 aliponyakua Kombe la Chama Cha Soka nchini Uingereza FA kitu ambacho kimemfanya aendelee kukosolewa kwa kiasi kikubwa sana.

Wenger ameweza kutwaa makombe matatu ya Ligi Kuu nchini Uingereza, makombe manne ya Kombe la FA pamoja na kuwa kocha Bora wa msimu wa ligi katika misimu mitatu ambayo ni 1998, 2002 na 2004.