ULAYA-UEFA

Bayern Munich yaishushia kipigo kizito Arsenal huku Porto ikipata ushindi mwembamba mbele ya Malaga

Klabu ya Arsenal ya nchini Uingereza imejiweka kwenye hatihati ya kusomga mbele kwenye Mashindano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya EUFA baada ya kukubalia kipigo cha nyumbani kutoka kwa Bayern Munich. Arsenal wamekubali kipigo cha nyumbani cha magoli 3-1 kutoka kwa Bayern Munich na hivyo kuzima matumaini yao ya kumaliza ukame wa mataji walionao tangu mwaka 2005 waliposhinda Kombe lao la mwisho.

Mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Mueller akifunga goli la pili kwenye mchezo wao dhidi ya Arsenal
Mshambuliaji wa Bayern Munich Thomas Mueller akifunga goli la pili kwenye mchezo wao dhidi ya Arsenal
Matangazo ya kibiashara

Bayern Munich wakicheza ugenini kwenye Dimba la Emirates walipata goli la kuongoza katika dakika ya saba kupitia Toni Kroos aliyepiga mkwaju uliomshinda golikipa wa Arsenal, Wojciech Szczesny.

Dakika kumi na nne baadaye Bayern Municha wakaendelea ubabe wao kwa kufunga goli la pili kupitia kwa Thomas Mueller matokeo ambayo yalidumu hadi dakika arobaini na tano zinamalizika.

Kipindi cha Pili Arsenal walionekana kuamka na hatimaye kupata goli kupitia kwa mchezaji wa zamani wa Bayern Munich Lukas Podolski lakini haikusaidia kwani Mario Mandzikic akaandika goli la tatu.

Kwa matokeo hayo Arsenal imeendelea kukabiliwa na mzimu wa kuwa na matokeo mabaya baada ya mwishoni mwa juma kupata kichapo kutoka kwa Blackburn Rovers na kuondolewa kwenye Kombe la Chama Cha Soka nchini Uingereza FA.

Mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya UEFA ulishuhudia Porto wakicheza nyumbani na kuibuka na ushindi wa goli 1-0 mbele ya Malaga na kujiweka katika nafasi nzuri ya kutinga hatua ya Robo Fainali.

Goli la Joao Moutinho alilofunga kipindi cha pili lilitosha kuwapa ushindi waliokuwa nyumbani kwenye uwanja wa Estadio do Dragao ambapo tangu mwaka 2009 hawajawahi kufungwa kwenye mashindano hayo.

Porto walitawala zaidi mchezo huo na kupoteza nafasi nyingi za kufunga lakini washambulizji wake hawakuwa makini kuweza kuzitumia na hivyo mchezo kumalizika kwa ushindi huo mwembamba.