UINGEREZA-UEFA

Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere amkingia kifua Kocha Wenger baada ya kichapo kutoka kwa Bayern Munich

Siku moja baada ya Klabu ya Arsenal ya nchini Uingereza kupata kipigo cha magoli 3-1 kwenye Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kutoka kwa Bayern Munich kiungo wake Jack Wilshere amekataa kuelekeza lawama kwa Kocha wao Arsene Wenger. Kiungo huyo Kinda Mahiri wa Arsenal Wilshere amesema Kocha Wenger hapaswi kunyooshewa kidole cha lawama kwa matokeo hayo na badala yake wachezaji wenyewe inabidi wawajibike kwa hilo.

Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere akiondoka uwanjani kwa masikitiko baada ya mchezo wao na Bayern Munich
Kiungo wa Arsenal Jack Wilshere akiondoka uwanjani kwa masikitiko baada ya mchezo wao na Bayern Munich
Matangazo ya kibiashara

Wilshere amesema kwa kipindi cha miaka 16 Wenger amefanyakazi yake ipasavyo hivyo hakuna sababu ya aina yoyote ya kuhoji kile ambacho anakifanya na huu ni wakati wa wachezaji kuonesha uwajibikaji wao.

Kiungo huyo amesema Kocha Wenger alifanya kazi yake vizuri nje ya uwanja na sehemu ambayo ilisalia ilikuwa ni kwa wachezaji wenyewe kuwajibika na kupata matokeo mazuri lakini haikuwa hivyo.

Wilshere amesema walianza mchezo huo vibaya na ndiyo maana wakajikuta wakiruhusu magoli mawili kwenye kipindi cha kwanza na walipoarekebisha makosa wakacheza vizuri na hata kupata goli moja.

Kinda huyo wa Kiingereza amesema lazima waweka wazi ukweli ambao kwa Klabu kama Arsenal haiwezi kupata matokeo mazuri kwa Timu bora kama Bayern Munich ambayo imesheheni wachezaji mahiri.

Kwa upande wake Wenger amesema wanakazi ngumu mbele yao ili waweze kufuzu katika hatua ya Robo Fainali kutokana na kuruhusu magoli kwenye mchezo huo wa kwanza waliocheza nyumbani.

Wenger hakusita kusema chochote kinaweza kikatokea kwa kipindi cha majuma mawili hayajayo na huenda wakapata nafasi ya kutinga Robo Fainali japokuwa ukweli ni vigumu sana kwao.

Arsenal imejiweka kwenye mazingira magumu ya kufuzu katika hatua ya Robo Fainali huku ikiwa na kumbukumbu ya kuondolewa kwenye Kombe la Chama Soka nchini Uingereza FA baada ya kupokea kipigo kutoka kwa Blackburn Rovers.