ITALIA-UTURUKI

AC Milan yaifunga Barcelona na kujiweka kwenye mazingira mazuri huku Galatasaray na Schalke 04 zikichoshana nguvu

Kiungo wa AC Milan Sulley Muntari akifunga goli la pili kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Barcelona
Kiungo wa AC Milan Sulley Muntari akifunga goli la pili kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Barcelona

Klabu ya AC Milan ya Italia imejiwekea mzingira mazuri ya kufuzu katika hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya baada ya kuchomoza na ushindi kwenye mchezo wa kwanza wa mtoafo dhidi ya Barcelona. AC Milan imejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu katika hatua ya Robo Fainali baada ya kutoa kipigo kwa Barcelona kwa magoli 2-0 katika mchezo ambao ulikuwa na ushindani muda wote wa mchezo.

Matangazo ya kibiashara

Rossoneri wakiwa kwenye Uwanja wao wa nyumbani wa San Siro walionekana kuwa watulivu muda mwingi wa mchezo wa kuwadhibiti vilivyo wachezaji wa Barcelona ambao walikosa umakini.

Kevin-Prince Boateng ndiye alikuwa wa kwanza kuandika goli kwa AC Milan akiunganisha mpira wa faulo uliopigwa kabla ya kumgonga mchezaji wa Rossoneri na ndipo mpira ukamrudia na kukwamisha nyavuni.

Dakika tisa kabla ya mchezo huo haijamalizika AC Milan wakajipatia goli la pili kupitia kwa Sulley Muntari aliyeunganisha mpira Stephan El Shaarawy na kuiweka timu yake katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

Milan walionekana kutawala zaidi mchezo huo na kusima mashambulizi yaliyokuwa yanapangwa na viungo wa Barcelona akiwemo Xavi Hernandez, Andres Iniesta na Lionel Messi.

Katika mchezo mwingine wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Galatasaray wametoshana nguvu na Schalke 04 kwa kwenda sare ya kufungana goli 1-1 katika mchezo uliotawaliwa na mashambulizi mengi.

Galatasaray ndiyo walikuwa wa kwanza kuandika goli kupitia Burak Yilmaz ambaye aliachia mkwaju mkali ulimshinda mlinda mlango Timo Hildebrand na hivyo kuwafanya waongoze.

Schalke 04 waliendelea mashambulizi hayo na hatimaye kupata goli la kusawazisha kupitia Jermaine Jones na hivyo kuweka matumaini yao hai katika mchezo wa marudiano ambao utapigwa nyumbani kwao Ujerumani.

Didier Drogba alirejea kwa mara ya kwanza katika mashindano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya tangu apige penalti ya mwisho kwenye mchezo wa fainali kuisaidia Chelsea kutwa taji mbele ya Bayern Munich hapo mwaka jana.