UINGEREZA

Kibarua cha Arsene Wenger kipo salama Arsenal licha ya kupata matokeo mabaya kwenye michezo yake iliyopita

Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger ameendelea kuhakikishiwa usalama wa kibarua chake licha ya kupata matokeo mabaya katika mechi za hivi karibuni na kujikuta amepoteza matumaini ya kutwa ubingwa wowote msimu huu. Wenger amekumbana na ukosoaji mkubwa baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Chama Cha Soka Nchini Uingereza FA kufuatia kupata kichapo kutoka kwa Blackburn Rovers lakini aliendelea kunyooshewa kidole cha lawama baada ya kufungwa na Bayern Munich.

Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger ambaye amehakikishiwa usalama wa kibarua chake Emirates
Kocha Mkuu wa Arsenal Arsene Wenger ambaye amehakikishiwa usalama wa kibarua chake Emirates
Matangazo ya kibiashara

Usalama wa kibarua cha Wenger kuendelea kusalia Emirates kukikonoa Kikosi cha Arsenal umekuja baada ya kutolewa kwa agenda za Bodi ya timu hiyo bila kuonekana ile ambayo inahusu mustakabali wa Kocha huyo.

Wenger anatarajiwa kuhudhuria kikao hicho kutokana na kuwa Mjumbe wa Bodi huku akijuafika hakutakuwa na agenda ambayo inahusu kumjadili yeye licha ya kuendelea na ukame wa kutwaa mataji tangu achukue Kombe la FA mwaka 2005 kwa mara ya mwisho.

Arsenal imeonesha haina mpango wa kutaka kumtimua Wenger kuendelea kukinoa Kikosi chake hata kama Kocha huyo atakosa nafasi ya kufuzu katika Mashindano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Mkurugenzi mwenye hisa kubwa zaidi ndani ya Arsenal, Stan Kroenke na Wakurugenzi wenzake wameendelea kutangaza kumuunga mkono Wenger licha ya kuendelea kuchechea kwa timu hiyo kwenye mashindano mbalimbali.

Wajumbe wa Bodi kwenye mkutano wao wanatarajia kujikita zaidi kuangalia nini cha kufanya ili kuhakikisha timu hiyo inamaliza ukame wa kutwa mataji ambao umeshuhudiwa kwa karibu miaka nane sasa.

Arsenal imeeleza inafahamu fika hasira walizonazo mashabiki wa timu hiyo lakini kwa sasa wanatengeneza mikakati itakayowafanya waweze kupambana na Klabu kubwa Barani Ulaya na kutwa mataji kama ilivyokuwa zamani.

Mkataba wa Wenger na Arsenal unatarajiwa kufika tamati mwaka 2014 na itakuwa ni maamuzi ya Kocha huyo kuamua kuongeza au kusitisha kandarasi ya kuendelea kusalia Emirates.