EUROPA-UINGEREZA-ITALIA

Kocha Mkuu wa Tottenham Villas-Boas aeleza wapo tayari kwa mchezo dhidi ya Inter Milan kwenye Europa

Kocha Mkuu wa Tottenham Hotspur Andre Villas-Boas amesema wapo tayari kukabiliana na Inter Milan kwenye mchezo wa Kombe la Europa baada ya kufuzu kwa kuiondoa Olympique Lyon. Villas-Boas amesema baada ya kuiondosha Lyon sasa wanaangalia mchezo ujao dhidi ya Inter Milan huku wakitambua fika wanakutana na moja ya vigogo wa soka Barani Ulaya lakini wanataka kushinda mchezo huo.

Kocha Mkuu wa Tottenham Andre Villas-Boas amejigamba kikosi chake kipo tayari kwa mechi dhidi ya Inter Milan
Kocha Mkuu wa Tottenham Andre Villas-Boas amejigamba kikosi chake kipo tayari kwa mechi dhidi ya Inter Milan
Matangazo ya kibiashara

Kocha huyo raia wa Ureno amesema hatua ya wao kupangwa na Inter Milan inawapa nafasi ya kuwa na matumaini ya kuweza kushinda Kombe la Europa iwapo watawaondoa kwa sababu ni kipimo tosha kwao.

Villas-Boas amekiri mchezo huo lazima utakuwa mgumu kutokana na wachezaji mahiri wanaounda kikosi cha Inter Milan lakini wao pia wana timu bora iliyofanikisha kuwaondoa Lyon.

Tottenham imefanikiwa kutinga hatua ya kumi na sita bora baada ya kupata sare ya ugenini mbele ya Lyon ya goli 1-1 huku wakinufaika zaidi na ushindi walioupata nyumbani wa magoli 2-1 na hivyo kufuzu kwa jumla ya magoli 3-2.

Gola la kusawazisha la Tottenham lilifungwa dakika za lala salama na kiungo raia wa Ubelgiji Moussa Dembele na kuzima ndoto za Lyon ambayo kama ingepata ushindi wa goli 1-0 ingesomba mbele.

Timu hizo mbili zitakutana huku Inter Milan ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa magoli 4-3 kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya miaka miwili iliyopita huku Gareth Bale akifunga magoli matatu.

Tottenham wakati huo ilikuwa inanolewa na Harry Redknapp lakini sasa ipo chini ya mwalimu mwingine ambaye amekuwa akimtumia Bale kama nguzo yake kwenye safu ya mashambulizi.