SOKA

Timu za Afrika zaingia katika maandalizi ya lala salama michuano ya kufuzu kwa kombe la dunia

Mataifa mbalimbali ya Afrika yameingia katika maandalizi ya lala salama kabla ya kucheza michuano ya soka kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Mechi kadhaa zinachezwa barani Afrika mwishoni mwa juma hili, Tanzania inajiandaa kumenyana na Morroco jijini Dar es salaam.

Kocha wa Taifa Stars Kim Poulsen amekitaja kikosi cha wachezaji 23 wanaojiandaa jijini Dar es salaam tayari kwa mchuano huo huku wachezaji wa klabu ya Azam FC waliokuwa wanashiriki katika mchuano ya shirikisho barani Afrika nchini Liberia wakitarajiwa kuripoti kambini  siku ya Jumanne.

Baadhi ya wachezaji wa kulipwa wanaotegemewa katika kikosi hicho ni pamoja Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaochezea TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemorasi ya Congo.

Nchini Kenya, kocha Adel Amrouche anasema ameridhika na kiwango cha wachezaji wake wengi wao wanaocheza soka nyumbani.

Amrouche amesisitiza kuwa hatishwi na kutokuwepo kwa wachezaji wote wa kulipwa kama inavyohitajika kuwa siku tano kabla ya mchuano wao dhidi ya Nigeria wawe wameshafika kambini.

Hata hivyo nahodha Dennis Oliech anayecheza soka ya kulipwa nchini Ufaransa amewasili katika kambi ya Stars kwa maandilizi ya mchuano huo dhidi ya Super Eagles  mjini Calabar siku ya Jumamosi.

Uganda Cranes chini ya kocha wao Bobby Williamson wameanza maadalizi yao jijini Kampala Jumatatu asubuhi kwa maandilizi dhidi ya Liberia siku ya Jumapili mjini Monrovia.

Kocha Williamson amesema kuwa atawatumia wachezaji wakongwe na wenye uzoefu kama kipa Dennis Onyango, Andy Mwesigwa, Geoffrey Massa na Hassan Wasswa katika kikosi chake kitakaochokuwa uwanjani.

Nchini Afrika Kusini wachezaji wa kutegemewa kama vile mshambulizi Siyabonga Sangweni, Tsepo Masilela wamepata majeraha wakati Bafanafana ikijianda kucheza dhidi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.