SOKA

Hatimaye serikali ya Tanzania yakubaliana na shirikisho la soka TFF kuhusu uchaguzi wa viongozi

Serikali ya Tanzania imekubali mchakato wa uchaguzi wa Shirikisho la soka nchini humo TFF uendelee na kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea waliofika mbele ya Kamati ya Rufani ya Uchaguzi huo .

Matangazo ya kibiashara

Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye kikao kati ya uongozi wa Wizara ya Michezo nchini humo chini ya Waziri Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa nchini humo.

Tenga anayemaliza muda wake amesema TFF italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu FIFA ambalo ndilo lililosimamisha mchakato huo ili litume ujumbe wake kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.

Aidha Tenga ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali na hakuna atakayefungiwa katika kinya'nga'nyiro hicho.

Rais huyo wa TFF amewataka wagombea wote waliofika kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na waendelea kujiandaa vizuri, kwani FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.

Shirikisho la soka duniani FIFA wiki mbili zilizopita ilikuwa imeionya TFF kuwa itaifungia ikiwa serikali ingeendela kuingilia maswala ya soka nchini humo.