SOKA

Kenya yawasili Lagos huku Tanzania ikiisubiri Morocco Ijumaa tayari kwa mechi za kufuzu kwa kombe la dunia 2014

Timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars imewasili jijini Lagos nchini Nigeria tayari kwa mchuano wa kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Super Eagles siku ya Jumamosi.

Matangazo ya kibiashara

Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuelekea mjini Calabar siku ya Alhamisi mji ambao mchuano huo utachezwa katika uwanja wa UJ Esuene .

Kikosi cha Stars chini ya Kocha Adel Amrouche kutoka Ubelgiji kimesema kina matumaini makubwa ya kunyakua ushindi ugenini huku wachezaji wa kulipwa wakiongozwa na nahodha wao Dennis Oliech anayecheza soka nchini Ufarana na Victor Wanyama anayechezea klabu ya Celtic nchini Scotland wote wakiahidi kuipa Super Eagles wakati mgumu.

Super Eagles ambao ni mabingwa wa soka barani Afrika kwa upande wao wamejinadi kuipa Harambee Stars kipigo nyumbani kwao na kurudi kwa mshambulizi Peter Odemwingie anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya West Bromwich nchini Uingereza akirejea katika kikosi cha Kocha Stephen Keshi.

Nayo Uganda Cranes inandoka Kampala siku ya Alhamisi kuelekea Monrovia kuchuana na  Liberia.

Kocha Bobby Williamson amewaacha nje ya kikosi chake cha mwisho  Daniel Sserunkuma, anayechezea klabu ya Gor Mahia ya Kenya, Brian Umony wa Azam FC ya Tanzania pamoja na Hamis ‘Diego’ Kiiza wa Yanga pia anayecheza nchini Tanzania.

Kwingineko. timu ya taifa ya Morocco inatarajiwa kuwasili nchini Tanzania siku ya Ijumaa tayari kwa mechi dhidi ya Taifa Stars siku ya Jumapili katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Nao mabingwa wa zamani wa soka barani Afrika Zambia wanajiandaa kumenyana na Lesotho huku nahodha wa Chipolopolo Christopehr Katongo akisema mchuano wao hautakuwa rahisi.

Timu tano barani Afrika zitafuzu kushiriki katika kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014.