SOKA

Misri yafuzu nusu fainali ya michuano ya soka baina ya chipukizi barani Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Misri yenye wachezaji walio chini ya umri wa miaka 20 imekuwa timu ya kwanza kufika nusu fainali ya michuano ya Afrika ya vijana chipukizi inayoendelea jijini Algers nchini Algeria.

Matangazo ya kibiashara

Misri ilifuzu katika hatua hiyo baada ya kuishinda wenyeji wa michuano hiyo Algeria bao 1 kwa 0 katika mchuano pili wa kundi lao, baada ya kushinda mchuano wa kwanza kwa kuifunga Ghana mabao 2 kwa 1.

Mbali na kufuzu katika hatua hiyo, Misri pia imefuzuku kucheza kombe la dunia kwa vijana chipukizi itakayoandaliwa nchini Uturuki kati ya mwezi Juni na Julai mwaka huu.

Misri inaongoza kundi la A kwa alama 6 baada ya kushinda mechi zake mbili huku Ghana ikiwa ni ya pili kwa alama 3 baada ya kushinda mchuano wake wa ufunguzi dhidi ya Benin kwa kuifunga bao 1 kwa bila.

Mechi za mwisho za kundi la A zitachezwa siku ya Ijumaa ambapo wenyeji Algeria ambao wako katika nafasi ya tatu kwa alama moja watacheza dhidi ya Ghana huku Benin wakichuana na Misri.

Mali itachuana na Jamhuri ya Kidemokarsia ya Congo wakati Gabon ikimenyana na Nigeria siku ya Jumatano katika mechi za kundi B.

Mataifa yatakayofika katika awamu ya nusu fainali yatawakilisha bara la Afrika katika michuano ya kombe la dunia.