Harambee Stars ya Kenya yapata mapokezi mabaya nchini Nigeria
Shirikisho la soka nchini Nigeria NFF limeipa mapokezi mabaya timu ya taifa ya soka ya Kenya Harambee Stars baada ya kuwasili mjini Lagos tayari kuchuana na Super Eagles siku ya Jumamosi katika mechi ya kufuzu kwa kombe la dunia mjini Calabar.
Imechapishwa:
Wachezaji wa Kenya walipowasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed mjini Lagos hakuna kiongozi wa shirikisho la soka nchini humo aliyekuwepo kuwapokea.
Kabla ya kufika Nigeria, uongozi wa Harambee Stars ulihakikishiwa kupata usafiri wa ndege ya kukodi moja kwa moja hadi mjini Calabar kwa maandalizi ya mchuano huo ahadi ambayo haikutimizwa na wenyeji wao.
Ujumbe wa Kenya ukiongozwa na Hussein Terry haukufaulu kuwasiliana na maafisa wa NFF ili kutafuta njia nyingine za usafiri kwenda mjini Calabar baada ya kuambiwa kuwa ndege waliyokuwa wamepangiwa ilikuwa imejaa.
Aidha, Kenya imelalamikia hoteli ambayo wachezaji wake walihifadhiwa na wenyeji wao kwa kile wanachokisema mazingira hayakuwa mazuri na ni kinyume na utaratibu wa shirikisho la soka duniani FIFA unaohitaji wenyeji wa mchuano wa Kimataifa kama huu kuhakikisha kuwa wachezaji wanalala katika hoteli nzuri yenye nyota nne.
Shirikisho la soka nchini Kenya FKF limeiandikia barua shirikisho la soka nchini Nigeria kutaka kuhakikisha kuwa vijana wa Stars wanapewa usalama wa kutosha wanapojiandaa kwa mchuano huo.
Harambee Stars wamekuwa wakifanya mazoezi yao katika uwanja wa shule ya msingi ya Ajao kwenye uwanja wa mchanga chini ya kocha wao Adel Amrouche.
Uongozi wa Harambee Stars umesema wachezaji wa Stars watatumia mapokezi hayo mabaya kusaka ushindi dhidi ya mabingwa hao wa Afrika kwa udi na uvumba.
Wachambuzi wa soka wanasema mapokezi kama haya huwa yanalenga kuwachosha wageni na kuwaathiri kisaikolojia kabla ya mchuano kama huo.