SOKA

Nigeria yajiongezea matumaini ya kufuzu nusu fainali ya michuano ya soka baina ya chipukizi barani Afrika

Timu ya taifa ya soka ya Nigeria ambayo ni bingwa mtetezi wa Afrika  katika michuano ya wachezaji wasiozidi umri wa  miaka 20 wamefufua matumaini ya kunyakua tena taji hilo baada ya kupata ushindi wa bao 1 kwa 0 dhidi ya Gabon katika mchuano wake wa pili uliochezwa Jumatano usiku katika uwanja wa Ahmed Zabana mjini Algers nchini Algeria.

Matangazo ya kibiashara

Nigeria walianza michuano hii vibaya kwa kufungwa bao 1 kwa 0 na Mali na ushindi huo unaiweka katika nafasi ya pili kwa alama  3 katika kundi hilo linaloongozwa na Mali ambayo ina alama 6 .

Mali iliifunga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mabao 2 kwa 1 na kudidimiza matumaini ya vijana wa Leopard wanaoshiriki kwa michuano hiyo kwa mara ya kwanza  kufuzu katika awali ya nusu fainali.

Baada ya Misri kufuzu katika nusu fainali ya michuano hiyo, Mali imekuwa timu ya pili kufuzu na tayari imefuzu pia kushiriki katika kombe la dunia katikati ya mwaka huu nchini Uturuki.

 

Misri inaongoza kundi la A kwa alama 6 baada ya kushinda mechi zake mbili huku Ghana ikiwa ni ya pili kwa alama 3 baada ya kushinda mchuano wake wa ufunguzi dhidi ya Benin kwa kuifunga bao 1 kwa bila.

Mechi za mwisho za kundi la A zitachezwa siku ya Ijumaa ambapo wenyeji Algeria ambao wako katika nafasi ya tatu kwa alama moja watacheza dhidi ya Ghana huku Benin wakichuana na Misri.

Mataifa yatakayofika katika awamu ya nusu fainali yatawakilisha bara la Afrika katika michuano ya kombe la dunia na sasa kazi inasalia kwa Ghana na Nigeria kushinda mechi zao zinazosalia ili kujihakishia nafasi ya kufuzu.