Mali kukosa huduma za wachezaji wake muhimu watakapomenyana na Rwanda Jumapili hii
Timu ya taifa ya soka ya Mali haitakuwa na wachezaji wanne wa kutegemewa katika mchuano wake wa kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Rwanda Jumapili hii.
Imechapishwa:
Mali itakosa huduma za wachezaji hao muhimu kama kiungo wa kati Samba Diakite, anayechezea klabu ya QPR ya Uingereza.
Wachezaji wengine ni pamoja na kipa Mamadou Samassa, Bakary Traore anayechea klabu ya AC Milan nchini Italia na Abdoulwhaid Sissoko wa Brest FC.
Amavumbi Stars ya Rwanda ilifungwa na Libya bao 1 kwa 0 katika mchuano wa Kimataifa wa kirafiki uliochezwa siku ya Jumatano usiku.
Mshambulizi matata wa Kigali Olivier Karekezi amesema kuwa licha ya kupoteza mchuano huo ana matumaini makubwa ya Amavumbi Stars kuibuka washindi katika mchuano wao wa siku ya Jumapili katika uwanja wa Amahoro.
Rwanda inahitaji kushinda mchuano huo ili kujiongezea matumaini ya kusonga mbele katika harakati za kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwaka ujao na ni ya mwisho katika kundi lao kwa alama moja.
Nayo timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo itachuana na Libya katika uwanja wa Kimataifa wa Stade de Martyrs jijini Kinshasa.
Libya itakuwa ugenini kutetea rekodi yake ya kutoshindwa katika michuano hiyo ambapo hadi sasa inaongoza kundi lao kwa alama nne baada ya ushindi na sare katika mechi zake mbili zilizopita.
Libya walianza kampeni zao kwa mguu wa kulia baada ya kuifunga Cameroon mabao 2 kwa 1 nyumbani na baadaye kulazimisha sare ya bao 1 kwa 1 na Togo mjini Lome.
Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo nayo ni ya pili katika kundi hilo na alama 3 baada ya kushinda mchuano wake wa kwanza na ikiwa itashinda mchuano wake dhidi ya Libya itaongoza kundi hilo ikiwa Togo itaishinda Cameroon.
DR Congo alimaarufu kama Leopard ambayo inaorodheswa ya 79 duniani ilifuzu kombe la dunia mara moja tu mwaka 1974.