WORLD CUP QUALIFYER-AFRIKA

Tanzania yaichapa Morocco mabao 3-1

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Sammata akiwatoka walinzi wa timu ya taifa ya Morocco
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Sammata akiwatoka walinzi wa timu ya taifa ya Morocco RFI

Michuano ya kuwania kufuzu kukata tiketi ya kucheza fainali za kombe la Dunia zitakazopigwa kule nchini Brazil mwaka 2014 kwa bara la Afrika zimeendelea siku ya Jumapili kwa timu mbalimbali kushuka viwanjani kuoneshana ubabe.

Matangazo ya kibiashara

Nchini Tanzania, timu taifa ya ya nchi hiyo Kilimanjaro Stars walikuwa wenyeji wa timu ya taifa ya Morocco kwenye mchezo ambao Tanzania walifanikiwa kuchomoza na ushindi mnono wa mabao 3-1.

Katika mchezo huo ambao kipindi cha kwanza kilimalizika kwa kila timu kushindwa kuliona lango la mwenzake, kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo wenyeji Tanzania ndio waliokuwa wa kwanza kuandika bao.

Goli la kwanza la Tanzania lilipatikana katika dakika ya 46 ya mchezo likifungwa na mchezaji wa kimataifa wa Tanzania anayekipiga na klabu ya TP Mazembe ya DRC, Thomas Ulimwengu, kabla ya dakika ya 67, mshambuliaji mwingine anayekipiga na timu ya TP Mazembe, Mbwana Samatta kuandika bao la pili.

Dakika ya 80 Mbwana Samatta tena aliipatia timu yake bap la tatu na laushindi ambapo wakati imesalia dakika moja mpira kumalizika, timu ya taifa ya Morocco walifanikiwa kuandika bao la kufutia machozi kupitia kwa Youssef El Arabi.

Katika mechi nyingine Ethiopia walikuwa wenyeji wa Botswana katika mchezo ambao ulishuhudia Ethiopia wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 na kufanikiwa kukaa kileleni mwa kundi A.

Mechi nyingine Equatorial Guinea walikuwa wenyeji wa timu ya taifa ya Cape Verde katika mchezo ambao Guinea waliibuka na ushindi mgumu wa mabao 4-3.

Lesotho wao walitoka sare ya bao 1-1 na Zambia wakati Ghana waifanikiwa kuchomoza na ushindi wa magoli 4-0 dhidi ya timu ya taifa ya Sudan.

Msumbiji wao wakatoka sare ya bila kufungana na Guinea, wakati timu ya taifa ya Rwanda wakalala nyumbani kwa kukubali kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Mali, huku DR Congo wakitoshana nguvu na timu ya taifa ya Libya.

Timu ya taifa ya Liberia yenyewe ikafanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabo 2-0 dhidi ya timu ya taifa ya Uganda.