WORLD CUP QUALIFICATIONS-UEFA

Uingereza yalazimishwa sare ya bao 1-1 na Montenegro, huku Ufaransa ikiangukia pua mbele ya Uhispania

Michuano ya kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia nchini Brazil kwa mataifa ya Ulaya, imeendelea usiku wa kuamkia leo kwa miamba kadhaa kushuka viwanjani kuoneshana ubabe.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania wakimkabili mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Karim Benzema
Wachezaji wa timu ya taifa ya Uhispania wakimkabili mshambuliaji wa timu ya taifa ya Ufaransa Karim Benzema Reuters
Matangazo ya kibiashara

Katika mechi ambayo ilikuwa inatazamwa ni ile iliyowakutanisha timu ya taifa ya Uhispania ambao walisafiri hadi nchini Ufaransa katika mchezo ambao umeshuhudia timu ya taifa ya Ufaransa ikiangukia pua kwa kukubali kipigo cha bao 1-0.

Goli pekee kwa nchi ya Uhispania lilipatikana katika kipindi cha pili cha mchezo kwenye dakika ya 58 likifungwa na mchezaji Pedro Rodriguez.

Mtanange mwingine ambao ulivuta hisia za mashabiki ni ile ya kundi H, ambapo timu ya taifa ya Uingereza walikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Montenegro kwenye mchezo ambao umeshuhudia timu hizo zikitoka sare ya bao 1-1.

Kwenye mchezo mwingine Ukrain walikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Moldovia na kushuhudia Ukrain ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, wakati timu ya taifa ya Poland ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya San Marino.

Mechi nyingine ilizikutanisha timu ya taifa ya Malta waliokuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Italia, mchezo ambao Italia iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, wakati Ujerumani yenyewe ikiibuka na ushindi wa magoli 4-1 dhidi ya Kazakhstan, huku Jamhuri ya Ireland ikitoshana nguvu na timu ya taifa ya Austria ya sare ya mabao 2-2.