CONCACAF-CONMEBOL-WORLD CUP

FIFA kuchunguza tukio lililomuhusisha Luis Suarez na Gonzalo wakati wa mechi ya Uruguay na Chile

Shirikisho la mpira wa miguu duniani FIFA limesema kuwa linachunguza tukio ambalo lilimuhusisha mshambuliaji wa Liverpool na timu ya taifa ya Uruguay Luis Suarez wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia dhidi ya Chile.

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uruguay, Luis Suarez Reuters
Matangazo ya kibiashara

Picha za video zilimuonesha mchezaji Luis Suarez akimpiga kiwiko mchezaji wa Chile Gonzalo Jara anayekipiga pia na timu ya Nottingham Forest ya Uingereza wakati wakiwania mpira kwenye kona ya uwanja.

Picha hizo zimeendelea kuwaonesha wachezaji hao wakijibizana kwa maneno na mwamuzi wa mchezo huo Nestor Pitana hakuchukua hatua zozote dhidi ya wachezaji hao.

FIFA imesema kuwa inasubiri kupata ripoti ya kamisaa wa mchezo ule ili kuendelea na na hatua zaidi za kiuchunguzi ambapo ikibainika walifanya makosa wachezaji hao watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Hata hivyo mwamuzi Pitina baadae alimpa kadi ya njano Suarez kwa kumkaripia mwamuzi, kadi ambayo itamfanya akose mchezo mwingine dhidi ya Venezuela.

Katika mchezo huo umeshuhudia timy ya Uruguay ikiangukia pua baada ya kukubali kipigo cha mabo 2-0 toka kwa Chile.

Kwa matokeo hayo yanaifanya Uruguay kuendelea kushikilia nafasi ya sita kwenye kundi lake la timu za Amerika Kusini zinazowania kukata tiketi ya kufuzu kucheza fainali za kombe la dunia nchini Brazil.

Katika matokeo mengine, Ecuador walichomoza na ushindi wa mabao 4-1 dhidi ya Paraguay, wakati Venezuela wakiibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Colombia.

Kwenye ukanda wa CONCACAF, timu ya taifa ya Costa Rica yenyewe ilifanikiwa kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Jamaica, wakati Panama nao wakichomoza na ushindi kama huo wa mabao 2-0 dhidi ya Honduras.

Katika mechi nyingine ya ukanda huo, timu ya taifa ya Mexico ilitoshana na nguvu na timu ya taifa ya Marekani ya kutokufungana.