UINGEREZA

Chelsea yatinga Nusu Fainali ya Kombe la FA baada ya kuiondosha Manchester United kwenye Robo Fainali

Mshambuliaji wa Chelsea Demba Ba akifunga goli dhidi ya Manchester United kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la FA
Mshambuliaji wa Chelsea Demba Ba akifunga goli dhidi ya Manchester United kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la FA

Matarajio ya Klabu ya Manchester United kushinda mataji katika msimu huu yametoweka rasmi baada ya kukubalia kichapo kutoka kwa Chelsea na hivyo kuondolewa kwenye hatua ya Robo Fainali ya Kombe la Chama Cha Soka FA. Manchester United imejikuta jahazi lake likizama mbele ya Chelsea katika mchezo uliopigwa dimbani Stamford Bridge na hivyo matarajio yao kuzama na sasa wanasalia kwenye kinyang'anyiro cha ligi pekee.

Matangazo ya kibiashara

Chelsea wamefanikiwa kuwaondoa Manchester United kwenye hatua ya robo fainali kwa goli pekee ambalo limefungwa na Mshambuliaji wa Kimataifa wa Senegal Demba Ba katika dakika ta arobaini na tisa.

Ba aliunganisha kifundi mpira mrefu uliopigwa na Kiungo wa Kimataifa wa Uhispania Juan Mata na mpira huo kumshinda mlinda mlango wa Manchester United David De Gea aliyeshindwa kuokoa.

Chelsea walionekana kujiamini katika mchezo huo licha ya kwenye ligi kuambulia kichapo mbele ya Southampton mwishoni mwa juma lakini mabadiliko ya wachezaji sita yaliwasaidia kufanya vizuri.

Kocha wa Manchester United Alex Ferguson alilazimika kuwaweka nje Robin Van Persie na Shinji Kagawa huku akiwaeka kwenye kikosi chake Danny Welbeck na Luis Nani lakini haikumsaidia kutokana na Chelsea walivyojiimarisha.

Kipa wa Chelsea Petr Cech ndiye alikuwa mchezaji bora kwa Chelsea kutokana na kuokoa magoli mawili ya wazi kutoka kwa mshambuliaji wa Kimataifa wa Mexico Javier Hernandez.

Chelsea walimpoteza beki wao wa kushoto Ashley Cole kutokana na kupata maumivu ya misuli lakini hata hivyo waliendelea kuonekana wakicheza vizuri hasa kwenye safu yao ya ulinzi.

Kufuatia ushindi ambao wameupata Chelsea kwenye mchezo huo wa marudiano wa Robo Fainali dhidi ya Manchester United wametinga nusu fainali na wanatarajiwa kukabiliana na Manchester City.

Mchezo wa nusu fainali wa Kombe la FA unatarajiwa kupigwa kwenye dimba la Wembley ambapo Mabingwa watetezi Chelsea watakuwa na kibarua cha kutetea taji lao mbele ya Manchester City.