UINGEREZA

Beki wa QPR Chris Samba awashukia mashabiki kuacha kujadili mshahara anaolipwa pindi akifanya makosa Uwanjani

Beki wa Kati wa QPR Chirs Samba akimdhibiti Mshambuliaji wa Fulham Dimitar Berbatov
Beki wa Kati wa QPR Chirs Samba akimdhibiti Mshambuliaji wa Fulham Dimitar Berbatov

Beki wa kati wa Klabu ya QPR Chris Samba amechukizwa na hatua ya kuendelea kusakamwa na mashabiki wa Timu hiyo ambao mara zote wamekuwa wakiujadili mshahara wake. Samba amewataka mashabiki wa QPR kuacha kuzungumzia mshahara wake ambao analipwa kila pale ambapo anafanya makosa uwanjani na amewataka wafahamu hata ni binadamu hivyo kuna wakati anakosea.

Matangazo ya kibiashara

Beki huyo wa Kati aliomba radhi kwa kosa alilolifanya kwenye mchezo dhidi ya Fulham ambapo alimwangusha Dimitar Berbatov kwenye eneo la penlati na mwamuzi kuamuru penalti ipigwe na kufungwa goli la kwanza.

Samba kupitia ukurasa wake wa twitter amewaambia mashabiki waangalie kile ambacho anakifanya uwanjani na si kuendelea kujadili mshahara ambao analipwa na Klabu ya QPR kwa sasa.

Beki huyo pia amekiri hakucheza vizuri kwenye kipindi cha kwanza cha mchezo dhidi ya Fulham ambao ulimalizika kwa QPR kuambulia kichapo cha magoli 3-2 huku moja likifungwa kwa mkwaju wa penalti.

Samba ambaye ni raia wa Jamhuri ya Congo ameshangazwa na kitendo cha mashabiki kuuzungumzia mshahara wake wa pauni laki moja ambao anavuna mwa wiki licha ya kujali mchango wake uwanjani.

Kocha wa QPR Harry Redknapp naye alionekana kuchukizwa na kipigo hicho na kusema hata Samba alishindwa kucheza katika mfumo ambao alipaswa kucheza na badala yake alikuwa anarudisha mipira nyuma badala ya kwenda mbele.

Redknapp amekiri kufungwa na Fulham kumeendelea kuiweka pabaya timu yake ya QPR ikiwa imesalia na michezo saba pekee kabla ya kumalizika kwa Ligi msimu huu na ndipo watajua hatima yao kama watabaki au watashuka daraja.

QPR imesalia na michezo dhidi ya Wigan Athletic, Everton, Stoke City, Reading, Arsenal, Newcastle United na mchezo wao wa mwisho utakuwa dhidi ya Liverpool ambao utapigwa kwenye dimba la Anfield.