EUFA-UJERUMANI-UFARANSA

Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kupigwa usiku wa leo

Mshambuliaji wa PSG Zlatan Ibrahimovic (Kusoto) na Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi (kulia) kabla ya mchezo wao usiku wa leo
Mshambuliaji wa PSG Zlatan Ibrahimovic (Kusoto) na Mshambuliaji wa Barcelona Lionel Messi (kulia) kabla ya mchezo wao usiku wa leo REUTERS/Gonzalo Fuente/Pepe Marin - Montage : RFI

Mkondo wa kwanza wa hatua ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya unaendelea usiku wa leo kwa kupigwa michezo miwili itakayowakutanisha Bayern Munich dhidi ya Juventus huku Paris St-German ikicheza na Barcelona. Bayern Munich watashuka dimbani kwenye Uwanja wake wa nyumbani kucheza na Kibibi Kizee cha Turin Juventus wakiwa na kumbukumbu nzuri ya kuibuka na ushindi mnono wa magoli 9-2 dhidi ya Hamburg.

Matangazo ya kibiashara

Munich watashuka dimbani kwenye Uwanja wa Allianz Arena kupimana ubavu na Juventus ambao nao walishinda mchezo wao wa mwishoni mwa juma wa ligi dhidi ya Inter Milan kwa magoli 2-1.

Kocha Mkuu wa Juventus Antonio Conte amesema watakabiliana na Bayern Munich bila ya hofu yoyote huku wakiwa na uhakika wa kuibuka na ushindi katika mcheo huo wa kwanza ili wajiwekee mazingira mazuri ya kufuzu nusu fainali.

Conte amewaambia wanahabari kikosi chake kipo tayari kukabiliana na timu ngumu ya Bayern Munich ili waweze kutimiza ndoto zao za kutinga nusu fainali na hatimaye kuibuka mabingwa mwaka huu.

Kocha wa Bayern Munich Jupp Heynckes hatarajii kama timu yake inaweza ikaibuka na ushindi mkubwa kama iliyoupata kwenye mchezo wa ligi ya Bundesliga lakini watahakikisha wanaibuka na ushindi.

Heynckes amesema wanafahamu fika watakumbana na upinzani mkali kutoka kwa Juventus lakini watalazimika kuutumia vyema uwanja wao wa nyumbani ili waweze kupata ushindi kwenye mchezo huo.

Mchezo mwingine utapigwa katika uwanja wa Parc des Princes ambapo miamba miwili Paris St-German watakumbana na Barcelona kusaka tiketi ya kutinga hatua ya nusu fainalia ya Ligi ya Mabingwa.

Barcelona wamesafiri kuelekea nchini Ufaransa wakiwa na wachezaji wao wote mahiri huku wakiwajumuisha wachezaji wao wawili waliokuwa majeruhi hapo kabla ambao ni Xavi Hanandez na Jordi Alba.

Wachezaji hao wote walikosa mchezo wa ligi nchini Ufaransa dhidi ya Celta Vigo ambao uliisha kwa matokeo ya sare ya magoli 2-2 na hivyo kuzua hofu huenda wangekosa mchezo huo wa leo.

Mshambuliaji wa PSG aliyewahi kucheza Barcelona Zlatan Ibrahimovic amesema wanapaswa kuwa makini na kuhakikisha wanaibuka na ushindi bila ya kuogopa kiwango cha wapinzani wao.