UEFA-UHISPANIA

Kocha wa Real Madrid Jose Mourinho atoa onyo kwa wachezaji wake kutobweteka na ushindi dhidi ya Galatasaray

Kocha Mkuu wa Real Madrid Jose Mourinho akiwa maelezo kwa wachezaji wake wakati wa mchezo ukiendelea
Kocha Mkuu wa Real Madrid Jose Mourinho akiwa maelezo kwa wachezaji wake wakati wa mchezo ukiendelea

Kocha Mkuu wa Real Madrid Jose Mourinho amekataa kuanza kusherehekea iwapo timu yake imeshafanikiwa kutinga hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya mabingwa Barani Ulaya licha ya kuvuna ushindi mnono wa magoli 3-0 mbele ya Galatasaray. Mourinho ametoa onyo kwa wachezaji wake kutoaamini wameshafuzu katika hatua ya Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa licha ya ushindi wao wa nyumbani walioupata usiku wa jana pale Santiago Bernabeu.

Matangazo ya kibiashara

Kocha huyo aliyebarikiwa tambo nyingi amesema bado wanakazi kubwa pindi watakapoenda Uturuki juma lijalo kukabiliana na wapinzani wao Galatasaray ambao huwa wanautumia vyema uwanja wao wa nyumbani.

Mourinho ameweka bayana wanapaswa kwenda Istanbul na kufunga goli moja kitu ambacho kitawafanya Galatasaray kuhitajika kushinda magoli matano ili wafuzu katika hatua ya Nusu Fainali.

Mourinho amesema kwenye mpira kitu chochote kinawezekana na hivyo ushindi wao bado si chochote hadi pale mchezo wa kondo wa pili wa robo fainali utakapomalizika huko Istanbul.

Kocha huyo wa zamani wa Chelsea amekisifu kikosi cha Galatasaray kuwa ni kigumu na kinacheza mchezo wa kujiamini mno na walionesha hilo licha ya kufungwa katika mchezo wa jana usiku.

Mourinho amewataka wachezaji wake kuendelea kuwaheshimu Galatasaray na kujiandaa vyema kwa ajili ya mchezo wa marudiano na kuwataka wacheze kwa nidhamu ya hali ya juu ili wawese kusonga mbele.

Kocha huyo hakusita kusema wataelekea Istanbul wakiwa na furaha kutokana kuvuna ushindi wao wa magoli 3-0 wakiwa nyumbani na amewashukuru mashabiki kwa namna ambavyo waliwaunga mkono.

Reald Madrid walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa magoli 3-0 mbele ya galatasaray kupitia kwa Cristiano Ronaldo, Karim Benzema na Gonzalo Higuani na kuonekana wamekaribia kutinga Nusu Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.