UINGEREZA-SOKA

Kocha wa Chelsea Benitez aridhishwa na kiwango cha Mshambuliaji wake Torres alichokionesha kwenye Europa

Mshambuliaji wa Chelsea Fernando Torres akishangilia goli alilofunga dhidi ya Rubin Kazan
Mshambuliaji wa Chelsea Fernando Torres akishangilia goli alilofunga dhidi ya Rubin Kazan

Kocha wa muda wa Klabu ya Chelsea Rafael Benitez ameanza kupata kiburi kutokana na Mshambuliaji wake Fernando Torres kuonesha makali ya kufunga kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Europa. Benitez ameanza kupata kiburi hicho kutokana na kiwango kilichooneshwa na Torres kwenye mchezo wa Robo Fainali ya Kombe la Europa ambapo timu hiyo ilipata ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya Rubin Kazan.

Matangazo ya kibiashara

Kocha wa Chelsea amesema ameridhishwa sana na kiwango kinachooneshwa na Torres katika michezo ya hivi karibu na ana uhakika ataendelea kusalia kwenye kiwango chake na kufunga magoli zaidi.

Benitez ambaye anapigana ili kuhakikisha Chelsea inatwaa taji la kombe la FA na Kombe la Europa amesema Torres amerea kwenye kiwango wakati muafaka ambapo mchango wake unahitajika zaidi.

Licha ya Torres kutofunga goli katika michezo ya Ligi Kuu nchini Uingereza tangu tarehe 23 ya mwezi Desemba lakini Benitez haoneshi kukerwa na hilo na badala yake kufunga kwake kwenye Europe kunampa faraja.

Benitez amepongeza hatua ya Torres kupigana kufa na kupona kutaka kuwa kwenye kikosi cha kwanza na matunda yake yameanza kuonekana baada ya kufunga katika mchezo huo wa Robo Fainali tena magoli mawili.

Kocha huyo wa muda amesema wataendelea kumtumia Torres pamoja na Demba Ba katika safu ya ushambuliaji kuhakikisha wanashinda mataji mawili wanayoyawania msimu huu kwa udi na uvumba.