RIADHA-BOSTON

Chama cha mchezo wa riadha duniani IAAF chalaani mashambulizi ya Boston

Chama cha mchezo wa riadha duniani IAAF kimelaani mashambulizi mawili ya mabomu yalitokea mjini Boston nchini Marekani wakati wa mashindano ya mbio ndefu na kusababisha vifo vya watu watatu na zaidi ya 100 kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa IAAF Lamine Diack ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya waliopoteza wapendwa wao kutokana na mashambulizi hayo na kutoa pole kwa waliojeruhiwa.

Diack amesema kuwa inashangaza kwa mtu kushambulia eneo kama hilo ambalo huwakutanisha watu na kuwashtumu watu waliotenda mashambulizi hayo kama wasio na  ubinadamu.

Nchini Uingereza, waandalizi wa mbio ndefu za London Marathon wamesema kuwa licha ya kutokea kwa mashambulizi hayo huko Boston mbio hizo zitaendelea kama ilivyopangwa Jumapili hii.

Waziri Mkuu David Cameroon amesema amesikitishwa mno  na mashambulizi hayo na kutoa salamu zake za pole kwa wale wote walioathiriwa na mkasa huo.

Rais wa Marekani Barrack Obama amesema kuwa lazima waliotekeleza mashambulizi hayo wachukuliwe hatua za kisheria, huku Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon akilaani tukio hilo wakati huu uchunguzi ukiendelea kubaini lengo la mashambulizi hayo waliotekeleza.

Shambulizi la kwanza lilitokea saa mbili baada ya washindi kuvuka mstari wa mwisho huku polisi wakiwa na wakati mgumu kuwasaidia wale waliokumbwa na milipuko hiyo.

Polisi mjini Boston wametoa wito kwa wakaazi wa mji huo kuepuka mikusanyiko ya watu wakati huu ambao bado hali ya usalama si ya kuridhisha kutokana na mashambulizi hayo.