SOKA-RWANDA

Micho afutwa kazi kama kocha wa Amavubi Stars ya Rwanda

Shirikisho la soka nchini Rwanda limemfuta kazi kocha wa timu ya taifa ya mchezo wa soka Milutin ‘Micho’ Sredojovic kutokana na matokeo mabaya ya Amavubi Stars katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.

Matangazo ya kibiashara

Katibu Mkuu wa chama cha soka Ferwafa, Michel Gasingwa amesema uamuzi huo wa kusitisha mkataba wa Micho wa miaka miwili umechukuliwa kutokana na kutoimarika kwa timu hiyo ya taifa katika michuano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo ile ya kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil.

FERWA inasema inasikitisha kuwa Amavubi Stars haijashinda kombe la Kanda Afrika Mashariki na Kati CECAFA kwa kipindi cha miaka miwili chini yake na kushindwa kufuzu kwa kombe la mataifa bingwa barani Afrika nchini Afrika Kusini,Gabon na Equitorial Guinea.

Kumekuwa na duru kuwa Micho ameomba kazi ya kuwa mkufunzi wa Uganda Cranes baada ya shirikisho la soka nchini Uganda FUFA kumfuta kazi kocha wake Bobby Williamson wiki iliyopita pia kwa sababu ya matokeo mabaya.

Awali, Micho raia wa Serbia pia alihusishwa wakati mmoja kuwa na mpango wa kujiunga na timu ya Kenya Harambee Stars bila mafanikio.

Wachambuzi wa soka katika kanda ya Afrika Mashariki na Kati wanasema kuwa Micho mwenye umri wa miaka 41 anaelewa vizuri soka ya Afrika Mashariki kutokana na kuwahi kufunza soka nchini Tanzania, Uganda, Ethiopia na pia Afrika Kusini na Yugoslavia.