SOKA

Cote dvoire yaiangusha Nigeria kwa ushindi mwembamba katika michuano ya Chipukizi

Timu ya soka ya Cote Dvoire ilipata ushindi wa bao 1 kwa 0 katika dakika za lala salama dhidi ya Nigeria katika mchuano wa kundi la B kuwania taji la bara Afrika baina ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 17 katika mashindano yanayoendelea nchini Morroco.

Matangazo ya kibiashara

Ushindi wa Cote Dvoire umeifanya kuendelea kuongoza kundi hilo kwa alama nne baada ya michuano miwili huku Nigeria ikiwa ya pili kwa alama tatu kutokana na ushindi wake mkubwa wa kwanza wa mabao 6 kwa 1 dhidi ya Ghana.

Congo Brazavile ilipata sare yake ya pili katika mashindano hayo ya bao 1 kwa 1 na Ghana, baada ya kupata sare kama hiyo na Cote dvoire katika mchuano wa ufunguzi na ni ya tatu katika kundi hilo kwa alama 2.

Ghana ni ya mwisho kwa alama moja na matumaini yao ya kufika katika hatua ya nusu fainali yanaonekana kudidimia huku wakisalia na mchuano mmoja.

Michuano ya mwisho ya kundi hili itachezwa siku ya Jumamosi kubaini timu zitakazofuzu katika awamu hiyo ya nusu fainali ambapo Congo watamenyana na Nigeria wakati Ghana wakimaliza kazi na Cote Dvoire.

Tayari wenyeji Morroco na jirani zao Tunisia wamefuzu katika nusu fainali itakayochezwa juma lijalo.

Timu zote nne zitakazofika katika awamu ya nusu fainali zitaliwakilisha bara la Afrika katika mashindano ya kombe la dunia yatakayofanyika katika Mmiliki za kiarabu kati ya tarehe 17 hadi tarehe 8 mwezi Novemba mwaka huu.