SOKA

Ferguson akanusha uvumi kuwa Wayne Rooney anaelekea Paris Saint-Germain

Kocha wa klabu ya soka ya Uingereza ya Manchester United Alex Ferguson amekanusha uvumi kuwa mshambulizi matata wa klabu hiyo Wayne Rooney yupo njiani kuhamia klabu ya Ufaransa ya Paris Saint-Germain.

Matangazo ya kibiashara

Kumekuwa na uvumi kuwa Rooney ambaye ni mchezaji wa Kimataifa wa Uingereza amekuwa akilengwa sana na klabu hiyo ya PSG licha ya kuwa na mkataba wa miaka miwili zaidi na klabu hiyo ya Old Trafford.

Ferguson ametoa kauli hiyo wakati timu yake inapojindaa kumenyana na Aston Villa siku ya Jumatatu juma lijalo katika mchuano ambao wakishinda huenda wakatawazwa kuwa mabingwa wa taji hilo.

Kipa wa Manchester United David De Gea aliyepata jeraha la kichwa wakati wa mchuano uliopita atashiriki katika mechi hiyo kwa mujibu wa Ferguson.

 

United walishindwa kujiongezea matumaini ya kujinyakulia taji hilo kabla ya ligi kukamilika baada ya kutoka sare ya mabao 2 kwa 2 na West Ham siku ya Jumatano usiku.

Hadi sasa, Manchester United inaongoza msururu wa ligi kwa alama 81 ikifuatwa na mabingwa watetezi Manchester City ambao wana alama 68 alama 13 nyuma ya United, huku nafasi ya tatu ikichukuliwa na Chelsea ambayo ina alama 61 baada ya kuishinda Fulham mabao 3 kwa 0.

Manchester City nao watatumai kuwa wataendelea kushinda mechi zote zilizosalia na kuomba Manchester United wanapoteza michuano yao yote ili kuona ikiwa wanaweza kutetea taji hilo.

Vlabu vya Chelsea, Tottenham Hotspurs, Asrsenal na Chelsea navyo vinawania kumaliza katika nafasi ya nne bora ili kushiriki kwenye mashindano ya kuwania taji la klabu bingwa barani ulaya UEFA.

Arsenal ni ya nne kwa alama 60, Spurs ni ya tano kwa alama 58 huku Everton ikiwa katika nafasi ya sita kwa alama 56.
Michuano ya mwisho ya ligi kuu nchini Uingereza itachezwa tarehe 19 mwezi ujao wa tano.