RIADHA

Mwanariadha Shawn Crawford kutoka Marekani afungiwa

Mwanariadha maarufu nchini Marekani Shawn Crawford aliyejinyakulia medali ya dhahabu katika mashindano ya Olimpiki mwaka 2004 katika mbio za mita 200 kwa upande wa wanaume amefungiwa kushiriki katika mashindano ya riadha kwa kipindi cha miaka miwili.

Matangazo ya kibiashara

Uamuzi huo umechukuliwa na taasisi ya kuchunguza utumizi wa dawa za kusisimua misuli ya marekani USADA baada ya mwanaridha huyo mwenye umri wa miaka 35 kukataa kushirikiana na taasisi hiyo.

Taasisi hiyo pia imetoa adhabu kwa mwanariadha kupokonywa mataji yote ambayo amewahi kushinda tangu mwezi Novemba mwaka 2012.

Mwaka 2008, Crawford pia alishinda mbio za mita 200 na zile za kupokonyana kijiti za mita 100 wakati wa mashindano ya Olimpiki nchini China mjini Beijing.

Mwaka 2004, Crawford alishinda mbio za mita 200 na kuweka rekodi bora ya sekunde 19 nukta 79 na kuwashinda Bernard Williams na Justin Gatlin.

Crawford hakufuzu katika mashindano ya Olimpiki ya mwaka 2012 baadaye ya kumaliza wa saba katika mashindano ya majaribio.