SOKA-ULAYA

Luis Suarez wa Liverpool aomba radhi baada ya kumng'ata beki wa Chelsea

AFP PHOTO

Mshambuliaji wa klabu ya soka ya Liverpool Luis Suarez ameomba radhi kwa kitendo alichokifanya katika mechi ya jumapili kati yao na Chelsea baada ya kumng'ata mlinda mlango wa Chelsea Branislav Ivanovic katika kipindi cha pili cha mchezo huo ambao ulimalizika kwa sare ya mabao mawili kwa kila upande.

Matangazo ya kibiashara

Akiwa katika dimba la Anfield, Ivanovic mwenye umri wa miaka 29 alilalamika kwa mwamuzi wa mechi hiyo Kevin Friend kuwa ameng'atwa na Suarez katika mkono wake wa kulia tukio ambalo mwamuzi hakuliona lakini limethibitika kupitia picha za video.

Kupitia mtandao wa kijamii wa twiter na facebook, Suarez mwenye umri wa miaka 26 amesema tayari ameongea na Ivanovic kwa njia ya simu na yupo tayari kukutana naye ili amuombe radhi moja kwa moja.

Katika taarifa yake ya awali Suarez amebainisha kuwa anaomba msamaha kwa Meneja wake na watu wote ndani ya klabu ya Liverpool kutokana na kosa alilolifanya.

Meneja wa Liverpool Brendan Rodgers amesema tabia iliyoonyeshwa na Suarez haikubaliki, na ameahidi hatua kuchukuliwa kwani hakuna mchezaji ndani ya klabu ambaye ana mamlaka ya juu kuliko utawala.

Hii si mara ya kwanza kwa Suarez kulalamikiwa kwa vitendo vya kuudhi katika mchezo wa soka na tukio la sasa hivi limesababisha Mkurugenzi wa klabu yake Ian Ayre kuahirisha safari yake ili kushughulikia suala hilo.