ITALIA-SERIE A

Juventus yatwaa Taji la 29 nchini Italia baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Palermo katika Ligi ya Serie A

Mabingwa Watetezi wa Italia Juventus wamefanikiwa kutetea Taji lao baada ya kuifunga Palermo katika mchezo waliokuwa wanahitaji pointi moja pekee ili waweze kutangazwa mabingwa mara ya 29. Goli la pekee la mkwaju wa penalti lililofungwa na Arturo Vidal lilitosha kuwapa ushindi Juventus maarufu kama Kibibi Kizee cha Turin kilichofanikiwa kutwaa taji hilo huku wakiongoza kwa tofauti ya pointi 14 mbele ya Napoli.

Wachezaji wa Juventus wakishangilia goli alilofunga Arturo Vidal kwenye mchezo dhidi ya Palermo
Wachezaji wa Juventus wakishangilia goli alilofunga Arturo Vidal kwenye mchezo dhidi ya Palermo
Matangazo ya kibiashara

Hii ni mara ya pili kwa Juventus kufanikia kutetea ubingwa wake huku mara ya kwanza kufanya hivyo ikiwa ni miaka kumi iliyopita lakini hii inazima mzimu wa wao kushushwa daraja mwaka 2006 wakituhumiwa kupanga matokeo.

Juventus kwa sasa inaongoza kwa kushinda mataji 29 ikiwa ni mataji kumi na moja zaidi kuliko timu inayoshika nafasi ya pili kwa kutwaa taji la Serie A na hivyo kudhihirisha ufalme wao kwenye soka la Italia.

Mchezo huo kati ya Juventus na Palermo ulishuhudia Kibibi Kizee hicho cha Turin kikilazimika kumaliza mchezo huo kikiwa na wachezaji 10 pekee baada ya kushuhudia Kiungo wale Paul Pogba akilimwa kadi nyekundu.

Hili linakuwa taji la tatu mfululizo kwa Andrea Pirlo ambaye alijiunga na Juventus akitokea AC Milan wakati huo wakiwa mabingwa watetezi huku yeye akisaidia kupatikana kwa taji hilo kabla hajahama.

Mafanikio haya ya Juventus yanaweza yakawa ni sawa kabisa na kutuma ujumbe kwa wale walioikashifu wakati ikishushwa daraja kwa makosa ya kupanga matokeo pamoja na Lazio na Fiorentina ambao wote wamekuwa wakifanya vizuri.