TENNIS-MADRID OPEN

Djokovic aondolewa kwenye Mashindano ya Madrid Open kwa kufungwa na Chipukizi Dimitrov

Mchezaji nambari moja wa Tennis Duniani upande wa Wanaume Novak Djokovic ameondolewa kwenye mzunguko wa pili wa mashindano ya Madrid Open baada ya kupewa kichapo kutoka kwa Grigor Dimitrov.

Mchezaji wa Tennis raia wa Bulgaria Grigor Dimitrov akirudisha mpira uliopigwa na Novak Djokovic
Mchezaji wa Tennis raia wa Bulgaria Grigor Dimitrov akirudisha mpira uliopigwa na Novak Djokovic
Matangazo ya kibiashara

Kichapo hicho kwa Djokovic kimewashtua wengi kutokana na kufungwa na mchezaji mchanga kutoka nchini Bulgaria, Dimitrov na kusitisha ndoto zake za kutwaa Taji la Madrid Open mwaka huu.

Djokovic kwenye mchezo huo alichapwa kwa jumla ya seti 2-1 kwa matokeo ya kufungwa seti ya kwanza kwa 7-6 kabla hajaibuka usingizini na kusinda kwa 7-6 katika seti ya pili na kukubali kichapo katika seti ya tatu kwa 6-3.

Mchezaji huo nambari moja Duniani upande wa Wanaume alilazimika kupatiwa matibabu wakati mchezo huo unaendelea baada ya kupata maumivu kwenye kifundo cha mguu kilichosababisha kushindwa kufanya vizuri.

Dimitrov alionesha umahiri mkubwa na ushindani wa hali ya juu kwa Djokovic ambaye kutokana na maumivu yaliyokuwa yanamkabili akashindwa kabisa kujibu mashambulizi yaliyokuwa yanaelekezwa kwake.

Baada ya mchezo huo Dimitrov ambaye ni mchezaji chipukizi amekiri huo ni ushindi mkubwa sana kwake na utaendelea kusalia kwenye historia ya maisha yake kutokana na kumfunga mchezaji bora duniani Djokovic.

Djokovic kwa upande wake amesema ataamua hatimaye yake ifikapo siku ya jumamosi ambapo atakuwa amejua maumivu aliyoyapata kwenye kifundo cha mguu kwenye mchezo huo.

Dimitrov ni mshindi mataji mawili ya Vijana lile la Wimbledon na US Open kwa mwaka 2008 huku wengi wakimtabiria atakuja kuwa mchezaji mahiri zaidi Duniani katika siku za usoni.