UINGEREZA-SOKA

Kocha wa Manchester United Sir Ferguson kubwaga manyanga kuinoa Timu hiyo mwishoni mwa msimu huu

Kocha wa Manchester Unites Sir Alex Ferguson akiwa na mataji aliyoshinda siku zilizopita
Kocha wa Manchester Unites Sir Alex Ferguson akiwa na mataji aliyoshinda siku zilizopita

Kocha Mkuu wa Manchester United Sir Alex Ferguson ametangaza ataachia wadhifa wake mwishoni mwa msimu huu baada ya kukinoa kikosi hicho kwa kipindi cha miaka 26 na kuipa mataji 13 ya Ligi Kuu nchini Uingereza. Sir Ferguson alijiunga na Manchester United tarehe 6 ya mwezi Novemba mwaka 1986 akirithi nafasi ya Ron Atkinson na kwa kipindi hicho chote amefanikiwa kutwaa mataji 38 katika muda huo wa miaka 26.

Matangazo ya kibiashara

Mataji ambayo ameshinda Sir Ferguson ni pamoja na mataji 13 ya Ligi Kuu nchini Uingereza, makombe mawili ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya, mataji matano ya Kombe la Ligi pamoja na Makombe matano ya Chama cha Soka FA.

Sir Ferguson mwenyewe amethibitisha uamuzi huo wa kujiuzulu wadhifa wake mwishoni mwa msimu huu na kusema kwake huu ni muda muafaka kuchukua uamuzi kama huo ya kukaa pembeni.

Kocha huyo mwenye heshima kubwa Old Trafford amesema ni muhimu kwake kuondoka sasa kutokana na kufanikiwa kujenga kikosi madhubuti ambacho kimefanikiwa kutwaa taji msimu huu mapema.

Sir Ferguson amekiri anajivunia vilivyo kuwa na kikosi imara ambacho kinawachezaji wenye wastani mzuri wa umri ambao wanaweza wakaisadia Manchester United kwa kipindi kirefu zaidi.

Kocha huyo mwenye msimamo madhubuti amesema anaondoka Old Trafford akiwa amechangia kuifanya timu hiyo kuwa na vifaa vyenye kiwango cha hali ya juu kwa timu kama Manchester United.

Sir Ferguson ametoa kauli hiyo baada ya kumaliza muda wa mazoezi asubuhi hii na kueleza anatoa shukurani za dhati kwa familia yake kwa ushirikiano waliokuwa wanampa kipindi chote na hasa mkewe Cathy.

Kocha huyo amesema kwa sasa anaangalia kuanza majukumu ya kuwa Mkurugenzi na Balozi wa Manchester United ili kuhakikisha anaendelea kuisaidia timu hiyo kupata mafanikio zaidi katika siku za usoni.

Mrithi wa Sir Ferguson ameanza kutajwa kuwa Kocha wa Everton David Moyes ambaye anamaliza muda wake wa kuinoa timu hiyo huku akiwa bado hajasaini mkataba mpya wa kuendelea kusalia Goodison Park.

Makocha wengine wanaotajwa kurithi nafasi ya Sir Ferguson ni pamoja na Jose Mourinho anayekinoa kikosi cha Real Madrid pamoja na Jurgen Klopp ambaye amepata mafanikio makubwa akiwa Borussia Dortmund.