UINGEREZA-SOKA

Manchester City yapata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya huku Wigan wakijichimbia kaburi ya kushuka daraja

Mshambuliaji wa Manchester City Edin Dzeko akifunga goli pekee dhidi ya West Brom
Mshambuliaji wa Manchester City Edin Dzeko akifunga goli pekee dhidi ya West Brom

Klabu ya Manchester City imefanikiwa kuweka kibindoni tiketi yake ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya kufuatia ushindi wa goli moja kwa nunge mbele ya West Bromwich Albino.

Matangazo ya kibiashara

Goli la pekee kwenye mchezo huo lilikwamisha nyavuni na Edin Dzeko na kutosha kabisa kumpa tiketi ya kushiriki Kombe la Ligi ya Mabingwa Roberto Mancini na kikosi chakekwa msimu wa pili mfulilizo.

Manchester City imefanikiwa kufikisha pointi sabini na tano na kujihakikishia kumaliza nafasi tatu za juu hata kama itafungwa katika michezo yake miwili iliyosalia na ipo nyuma kwa pointi kumi kwa mabingwa Manchester United.

Mchezo huo ulishuhudia wachezaji wa Manchester City wakiwa na uchu wa kuibuka na ushindi huku Carlos Tevez, Dzeko na Jack Rodwell ambao walishindwa kutumia nafasi kadhaa zilizotengenezwa na timu hiyo.

Manchester City wanajiandaa kushuka dimbani kwenye mchezo wa Fainali ya Kombe la FA dhidi ya Wigan Athletic ambao unatarajiwa kupigwa siku ya jumamosi kwenye dimba la Wembley.

Katika mchezo mwingine Wigan walijiweka katika hatari ta kushuka daraja msimu huu baada ya kukubalia kichapo cha nyumbani dhidi ya Swansea City cha magoli matatu kwa mawili mchezo uliopigwa usiku wa jana.

Wigan walikuwa wa kwanza kupata goli kwenye mchezo huo uliopigwa katika Dimba la DW kupitia Roger Espinoza kabla ya Swansea hawajasawazisha kwa goli lililofungwa na Angel Rangel.

James McCarthy akarejesha matumaini ya Wigan kuibuka na ushindi baada ya kufunga goli la pili lakini Swansea wakasawazisha kupitia Itay Shechter kabla ya Dwight Tiendalli kukwamisha goli la tatu.

Wigan kwa kichapo hicho imeendelea kusalia katika nafasi ya kumi na nane kwenye msimamo wa Ligi ikiwa imesalia na michezo miwili pekee kabla ya msimu kutamatika na kujua hatima yao iwapo watashuka daraja au la.

Kocha wa Wigan Roberto Martinez amesisitiza kuwa watafanikiwa kupata pointi tatu ili kujiondoa kwenye hatari ya kushuka daraja katika michezo yao miwili iliyosalia msimu huu.