UINGEREZA-SOKA

Mchuano wa kusaka nafasi ya kufuzu Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya wazidi baada ya Chelsea kutoka sare na Tottenham

Ushindani umeendelea kuwa mkali katika kusaka nafasi ya tatu na ya nne kwenye Ligi Kuu nchini Uingereza kwa timu tatu kuendelea kuchuana vikali baada ya Chelsea na Tottenham kumaliza mchezo wao kwa sare ya magoli 2-2.

Mshambuliaji wa Tottenham Gylfi Sigurdsson akifunga goli la kusawazisha dhidi ya Chelsea
Mshambuliaji wa Tottenham Gylfi Sigurdsson akifunga goli la kusawazisha dhidi ya Chelsea
Matangazo ya kibiashara

Tottenham walifanikiwa kusawazisha mara mbili ili kuweza kujinusuru na kichapo kutoka kwa Chelsea ambayo nayo inaendelea kusaka nafasi mbili zilizosalia kufuzu katika Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.

Chelsea walikuwa wa kwanza kupata goli kupitia mshambuliaji raia wa Brazili Oscar akiunganisha mpira uliopigwa na Gary Cahill na kuipa uongozi wa mapema kabla ya Emmanuel Adebayor hajasawazisha.

Kiungo wa Kimataifa wa Brazil Ramires akafunga goli la pili kuisaidia Chelsea kuongoza goli ambalo lilidumu hadi dakika arobaini na tano za kwanza zilipomalizika huku The Blues wakiwa vinara.

Kipindi cha pili kilishuhudia kila upande ukiendelea kupanga mashmbulizi yake kwa umakini mkubwa ambapo Chelsea walionekana wakihaha kusaka goli la tatu huku Tottenham wakitafuta goli la kusawazisha.

Dakika kumi kabla ya kumalizika kwa mchezo huo uliopigwa Stamford Bridge ukashuhudia Tottenham ikisawazisha kupitia mshambuliaji wake Gylfi Sigurdsson na kurejesha matumaini yao ya kupata nafasi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya msimu ujao.

Matokeo hayo yameongeza ushindani mkubwa katika kusaka nafasi hizo mbili zilizosalia za kufuzu kwa Mashindano ya Kombe la Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya baada ya manchester United na Manchester City kuchukua nafasi mbili.

Chelsea imeendelea kusalia katika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 69 huku Arsenal ikishikilia nafasi ya nne ikiwa imejikusanyia pointi 67 huku Tottenham ikiwa imeshaweka kibindoni jumla ya pointi 66.

Timu hizo zote mbili zimebakiwa na michezo miwili kabla ya msimu haujafikia tamati huku Manchester United akiwa ameshatwaa Ubingwa wa msimu huu mapema na kufikisha taji lake la 20.