ULAYA-ASIA

Polisi nchini Singapore yaendelea kumuhoji mtuhumiwa mkuu wa upangaji wa matokeo ya mechi barani Ulaya

Ulaya imekumbwa na kashfa ya upangaji matokeo
Ulaya imekumbwa na kashfa ya upangaji matokeo Reuters

Mamlaka nchini Singapore zimeanza kumuhoji mtuhumiwa mkuu wa upangaji wa matokeo ya mechi za mpira wa miguu barani Ulaya katika nchi tatu tofauti ikiwemo mechi thelathini na mbili.

Matangazo ya kibiashara

Mtuhumiwa huyo Dan Tan ambaye jina lake halisi ni Tan Seet Eng anashtakiwa pia na mahakama nchini Hungury kwa tuhuma kama hizo za kushiriki upangaji wa matokeo kwenye mechi za ligi hizo zaidi ya 20.

Juma moja lililopita polisi nchini Hungury zilimfungulia kesi rasmi ya upangaji matokeo kwenye mechi za mpira wa miguu na mahakama kutoa hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa Tan.

Kwenye taarifa iliyotolewa hii leo na mamlaka nchini Hungury na zile za Singapore, imesema kuwa kwa pamoja wameanza kufanya mahojiano na mtuhumiwa huyo pamoja na watuhumiwa wengine wakiwemo waamuzi na wachezaji mpira ambao walikamatwa kwa makosa ya kupanga matokeo.

Tan pia anatakiwa nchini Italia na Finland ambapo kwa nchi ya Hungury pekee watu zaidi ya 44 wamekamatwa na polisi maalumu wa kupambana na michezo haramu ikiwemo ya kupanga matokeo ya mechi kujipatia fedha kinyume cha sheria.

Mwanzoni mwa mwaka huu polisi wa Interpol barani Ulaya walitoa taarifa za siri ambazo zimewataja wachezaji mpira, timu na waamuzi kushiriki kwenye njama za kupanga matokeo na kutangaza kuanzisha uchunguzi rasmi dhidi ya watu hao.

Tan ni miongoni mwa wacheza kamari ambao uchunguzi wa awali umebaini kuwa alikuwa amepanga njama zaidi za kupanga matokeo kwenye mataifa mengi zadi duniani kabla ya mtandao wao kugunduliwa na polisi wa Interpol.

Hivi karibuni polisi maalumu wa Ujerumani walitembelea nchini Singapore na kufanya mahojiano na mtuhumiwa huyo ikiwa ni njia ya kubadilishana taarifa.