FRENCH OPEN

Novak Djokovic aendelea kutamba kwenye michuano ya French Open

Mchezaji nambari moja kwa mchezo wa tennesi duniani, Novak Djokovic
Mchezaji nambari moja kwa mchezo wa tennesi duniani, Novak Djokovic Reuters

Michuano ya tennesi ya French Open imeendelea kushika kasi jijini Paris Ufaransa huku ikishuhudiwa mchezaji nambari moja wa mchezo huo Novak Djokovic akisonga mbele kwa kishindo.

Matangazo ya kibiashara

Kwenye mchezo wake uliopigwa hiyo jana, Dojokovic alidhihirisha kuwa yeye ni bora zaidi duniani baada ya kumchakaza vilivyo mchezaji David Goffin kwa seti tatu bila kwa matokeo ya 7-6, 6-4 na 7-5.

Mara baada ya mchezo huo Djokovic licha ya kupata ushindi alimpongeza mpinzani wake na kukiri kuwa mashindano ya mwaka huu huenda yakawa magumu zaidi kuliko yale yaliyotangulia.

Kwenye mchezo mwingine mchezaji Fernando Verdasco alifanikiwa kusonga mbele baada ya kumshinda Marc Gicquel kwa seti tatu bila kwa matokeo ya 6-2, 6-3 na 6-1 kwenye mchezo ambao Verdasco aliutawala vilivyo.

Mchezaji nambari tisa kwa ubora wa mchezo huo, Stanislas Wawrinka alifanikiwa kuchomoza na ushindi dhidi ya Thiemo de Bakker, wakati Nikolay Davydenko akisonga mbele kwa kumfunga Florent Serra.

Kwa upande wa wanawake mchezaji Jelena Jankovic alifanikiwa kusonga mbele baada ya kuibuka na ushindi dhidi ya Daniela Hantuchova kwa seti mbili bila kwa matokeo ya 6-4 na 7-6.

Kwenye mchezo mwingine mchezaji, Samantha Stosur alimfunga Kimiko Date Krumm na kusonga mbele.