UINGEREZA

Mark Hughes atangazwa kuwa kocha mpya wa klabu ya Stoke City

Kocha mpya wa Stoke City, Mark Hughes
Kocha mpya wa Stoke City, Mark Hughes Reuters

Hatimaye Mark Hughes ametangazwa kuwa kocha mkuu wa timu ya Stoke City ikiwa ni miezi sita imepita toka atimuliwe kwenye kibarua chake cha awali na timu ya QPR iliyoshuka daraja msimu huu.

Matangazo ya kibiashara

Hughes anachukua mikoba ya raia mwenzake wa Wales, Tony Pulis ambaye alitangaza kuacahana na klabu hiyo kwa makubaliano maalumu baada ya kuitumikia kwa zaidi ya miaka saba.

Kocha huyu wa zamani wa klabu ya Manchester City amekuwa nje ya uwanja bila ya kufundisha timu yoyote toka mwezi November mwaka jana aliptimuliwa kazi kama bosi wa timu ya QPR.

Wakati akiwa na klabu ya QPR Hughes alijikuta kwenye wakati mgumu baada ya kujikuta timu yake ikishinda michezo nane pekee kati ya mechi 34 ambazo alikuwa amecheza hali iliyoufanya uongozi wa timu hiyo kumfuta kazi.

Nafasi yake ilizibwa na aliyekuwa kocha wa Tottenham Hotspurs, Harry Redknapp ambaye nae alishindwa kuinusuru timu hiyo na kushuka daraja licha ya kuendelea na kibarua chake kama kocha mkuu wa QPR.

Uongozi wa Stoke City unatarajiwa kumtangaza mbele ya waandishi wa habari kocha huyo maajira ya saa tano za asubuhi kwa saa za jiji la London Uingereza ambapo atatia saini mkataba wa miaka mitatu.

Mwenyekiti wa klabu hiyo Peter Coates amemsifu Hughes kwa kazi yake iliyotukuka kwenye masuala ya kabumbu na kuongeza kuwa huu ni wakati muafaka wa timu hiyo kupata kocha mwenye mapenzi na soka.