KOMBE LA DUNIA 2014-BRAZIL

Mechi ya kirafiki kati ya Uingereza na Brazil kuchezwa kama ilivyopangwa licha ya hofu ya kiusalama kwenye uwanja wa Maracana

Uwanja wa Maracana ambao utatumiwa leo kwenye mechi kati ya Brazil na Uingereza
Uwanja wa Maracana ambao utatumiwa leo kwenye mechi kati ya Brazil na Uingereza Reuters

Mechi ya kimataifa ya kirafiki baina ya timu ya taifa ya Uingereza na Brazil iliyopangwa kupigwa mjini Rio de Janeiro itachezwa kama ilivyopangwa licha ya hofu ya kiusalama kwenye uwanja wa Maracana.

Matangazo ya kibiashara

Siku ya alhamisi jaji wa mahakama moja mjini Rio aliagiza uwanja huo kutotumika kwa mechi hiyo ya kirafiki lakini baadae jaji mwingine alitengua uamuzi wa awali na kuruhusu mechi hiyo kupigwa kwenye dimba la Maracana.

Hofu ya kiusalama kuhusu uwanja huo ilitolewa na polisi na jopo maalumu lililokagua uwanja huo na udai kuwa ulikuwa na mapungufu ya kiusalama licha ya hivi karibuni kufanyiwa marekebisho.

Serikali ya Brazil hii leo nayo imetoa ripoti yake ikieleza kuwa imeridhishwa na taarifa mpya kuhusu uwanja huo na kwamba hakuna hofu tena ya kutumika kwa uwanja huo ambao pia utatumiwa wakati wa michuano ya kombe la shirikisho.

Uwanja wa Maricana ulifunguliwa mwezi April mwaka huu baada ya kuwa kwenye maetengenezo kwa karibu miaka mitatu na unauwezo wa kubeba mashabiki wa soka elfu sabini na nane wakiwa wamekaaa.

Wachambuzi wa masuala ya soka wamekosoa kamati ya maandalizi ya kombe la dunia nchini humo ambao wanadaiwa kushindwa kusimamia ujenzi wa haraka wa viwanja ambavyo vitatumika wakati wa fainali za kombe la dunia mwaka 2014.

Kumekuwa na hofu iwapo nchi ya Brazil imejiandaa vya kutosha kuandaa fainali hizo kwakuwa viwanja vingine vimeonekana kutokamilika ndani ya muda uliokuwa umepangwa na shirikisho la kabumbu dunia FIFA.