SOKA

Messi akana madai ya kutolipa kodi nchini Hispania

Mchezaji wa Kimataifa wa Argentina ambaye pia anacheza soka la kulipwa katika klabu ya Barcelona ya Uhispania Lionel Messi amekanusha madai kuwa yeye na baba yake Jorge Horacio Messi wamekuwa wakikwepa kulipa kodi inayokadiriwa kufikia zaidi ya Euro Milioni 4 kuanzia mwaka 2007.

Matangazo ya kibiashara

Messi mwenye umri wa miaka 25 ambaye ni mchezaji bora duniani kwa mwaka wa nne sasa, amesema ameshangazwa mno na madai hayo ya maafisa wa Uhispania wanaoshughulikia kodi.

Messi amesistiza kuwa yeye na babake wamekuwa wakilipa kodi kama inavyohitajika na serikali ya Uhipania na hawajawahi hata siku moja kukwepa kufanya hivyo suala ambalo anasema linaweza kuthibitishwa na wakala wake.

Messi na babake wamesema kuwa wao hawafahamu lolote na walipokea taarifa hizo kupitia vyombo vya habari kwa kile wanachosisitiza kuwa hakuna yeyote aliyewahi kujitokeza na kudai hawajalipa kodi.

Maafisa wanaoshughulika na kodi wamewasilisha kesi dhidi ya Messi na babake  katika Mahakama ya Catalonia anakoishi ili  kujibu mashtaka hayo wakati huu uchunguzi dhidi yake ukiendelea.

Kiongozi wa Mashtaka katika Mahakama hiyo anasema kuwa Messi na babake wamekuwa wakihusika na mpango huo kuanzia mwaka 2007 baada ya mbinu hiyo kuanza kupangwa mwaka 2005 wakati Messi alipokuwa na umri wa miaka 18.