SOKA

Super Eagles kuelekea Brazil Jumamosi baada ya kumaliza mgomo wa marupurupu

Mabingwa wa soka barani Afrika Nigeria walishindwa kusafiri kwenda Brazil siku ya Alhamisi kwa maandalizi ya kombe la dunia baina ya mabingwa wa mashirikisho baada ya kuzuka kwa malumbano kati yao na viongozi wa soka kuhusu marupurupu yao.

Matangazo ya kibiashara

Wachezaji wa Super Eagles walikataa kupanda ndege baada ya kutolipwa marupurupu waliokuwa wameahidiwa na shirkisho la soka la Nigeria NFF baada ya mchuano wao wa kufuzu kwa kombe la dunia dhidi ya Namibia siku ya Jumatano.

NFF ilikuwa imeahidi kuwalipa wachezaji hao Dola 5,000 baada ya mchuano huo na badala yake baada ya mchuano huo kumalizika na kutoka sare ya bao 1 kwa 1 wachezaji hao walilipwa Dola 2,000.

Rais wa Shirikisho la soka nchini Nigeria Aminu Maigari alikutana na wachezaji hao na kujaribu kuwashawishi wakubali nusu ya ahadi hiyo kwa sababu shirikisho hilo halikuwa na fedha ya kutosha kuwalipa kiasi walichokuwa wameahidiwa lakini wachezaji hao walikataa kupokea na kuelekea Brazil.

Wizara ya michezo ililazimika kuingilia kati mzozo huo na kuahidi kuwa wachezaji hao watalipwa marupurupu yao yote kama ilivyokuwa imeafikiwa na sasa Super Eagles watasafiri Brazil siku ya Jumamosi kwa maandalizi ya michuano hiyo.

Nigeria wamejumuishwa katika kundi moja na Tahiti, Uruguay na mabingwa watetezi wa taji hilo Uhispania na mchuano wao wa ufunguzi utakuwa na Tahiti siku ya Jumatatu.