ZAMBIA

Kenya yatoka sare na Lesotho kwa Magoli 2-2

Kikosi cha Timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars
Kikosi cha Timu ya Taifa ya Kenya Harambee Stars

Baada ya kulazimisha sare ya mabao 2 kwa 2 na Lesotho katika mchuano wa ufunguzi kuwania taji la soka baina ya Mataifa ya Kusini mwa Afrika COSAFA mjini Kitwe siku ya Jumatano, Kenya inashuka dimbani Jumanne hii kumenyana na Swaziland.

Matangazo ya kibiashara

Mbali na Lesotho na Swaziland , Kenya ambayo inashiriki katika mashindano haya kwa mara ya kwanza wamejumuishwa katika kundi moja na Bostwana.

Mataifa yote katika kundi hilo yana alama moja baada ya zote kutoka sare katika michuano ya ufunguzi wa mashindano hayo.

Mbali na Kenya mchuano mwingine unaochezwa Jumanne jioni ni kati ya Bostwana ambao wanamenyana na Lesotho katika uwanja wa Arthur Davies.

Mshindi katika kundi hili atafuzu katika duru ya robo fainali na kumenyana na Angola ambayo tayari imefuzu pamoja na wenyeji wa mashindano haya Zambia, nchi nyingine ni Msumbuji , Malawi, Afrika Kusini na mabingwa watetezi Zimbabwe.

Namibia wanaongoza kundi la A kwa alama 6 baada ya kushinda mechi zao zote kwa kuwachapa Mauritius mabao 2 kwa 1 huku wakiwacharaza Ushelisheli mabao 4 kwa 2 siku ya Jumatatu.

Namibia imefuzu katika hatua ya robo fainali na watamenyana na Afrika Kusini siku ya Jumamosi, huku mabingwa watetezi Zimbabwe wakimenyana na Malawi.

Siku ya Jumapili Angola watamenyana na mshindi wa kundi B huku wenyeji Zambia wakimaliza kazi dhidi ya Msumbuji.

Mechi za nusu fainali zitachezwa terehe 17 mwezi huu huku fainali ikiwa tarehe 20.